Lowassa Aibukia Nanenae Morogoro na Kutoa Ushauri Mzito Kwa Wakulima

WANANCHI wametakiwa kutumia tafiti zilizopo ili kuboresha kilimo kuwa cha kisasa na chenye tija ili kiweze kuwakwamua na umaskini.
Ushauri huo ulitolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa baada ya kutembelea mabanda kwenye uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Mwalimu J. K. Nyerere mjini Morogoro juzi.


Lowassa alieleza kuvutiwa na mafanikio makubwa na ubunifu kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza zaidi katika maonyesho hayo siku za usoni kwa kujifunza.


Aidha, Lowassa aliwashauri vijana kutumia maonyesho kama hayo kuwasilisha tafiti walizozifanya katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ili Watanzania wengi waweze kuzitumia kwa manufaa ikiwamo kujifunza na kubadilisha utendaji wa mazoea na kuwa wa kisasa kwa faida yao na taifa.


Lowassa alisema maendeleo duniani yanafikiwa kutokana na tafiti na kushauri kama Watanzania watatumia vyema matokeo ya tafiti zinazoendelea kufanywa na wataalamu, wataweza kufika mbali.


Katika ziara hiyo Lowassa alivutiwa na banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambamo alipongeza shughuli za uzalishaji wa kisasa wa mazao mbalimbali ikiwamo mboga.


JKT ilikuwa ikionyesha kilimo cha kutumia nyumba ya kijani (green house), ufugaji wa kisasa wa mbuzi wa maziwa, kuku, uvuvi na teknolojia nyingine zinazohusu sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.


Maonyesho hayo ambayo kitaifa yalikuwa mkoani Lindi, yalifikia kilele jana kwa kuhutubiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top