Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amemuandikia waraka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akimsihi kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa nchini bila kujali mipaka ya majimbo.
Lema amepaza sauti yake kupitia waraka wake kwa Rais Magufuli, uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, waraka ambao alithibitisha kuwa ni wake.
Katika waraka huo, Lema ambaye pia na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alimsihi Rais Magufuli kuviruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano hiyo kwani ni sehemu ya matakwa ya katiba.
Alitahadharisha kuwa endapo mambo yaliyoruhusiwa kikatiba hayataruhusiwa, ipo siku amri za utekelezaji wa masuala muhimu kikatiba hazitachukuliwa kwani hakutakuwa na sababu ya kuheshimu katiba na utawala wa sheria.
“Kama hatuwezi kufanya tunayoruhusiwa na Katiba, na anayetuzuia mamlaka yake yametokana na Katiba, hakika mbegu inayopandwa ni hatari kwa ustawi wa Taifa, ipo siku amri ya utekelezaji juu ya masuala muhimu haitachukuliwa kwa sababu umuhimu wa kuheshimu katiba na utawala wa Sheria hautakuwepo,” aliandika.
Lema alimueleza Rais Magufuli kuwa Siasa ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na kwamba mfumo huo ndiyo chanzo cha madaraka waliyonayo hapa nchini.
“Mheshimiwa Rais, siasa ni kazi na ndiyo maana wewe ni rais kwa sababu ya siasa, na mimi ni mbunge kwa sababu ya siasa, tena ni kazi muhimu sana tu kwani ndio mfumo pekee unaotafuta utawala wa ngazi mbalimbali na wa juu kabisa katika nchi,”
Aidha, Lema alimsemea kwa Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekitiwa CCM, Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka kwa kukiuka amri aliyoitoa Rais kwa kufanya mkutano Longido ambako sio jimbo lake.
“Mheshimiwa Rais, jambo hili litaleta mpasuko katika taifa letu, ni kauli inayopaswa kurekebishwa haraka. Hivi karibuni, msemaji wa CCM, Ole Sendeka alifanya mkutano Longido. Je, Ole Sendeka ni Mbunge wa Longido? Au polisi wa Mkoa wa Arusha hawakusikia tamko lake? "Alihoji.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa Chadema itafanya maandamano Septemba Mosi mwaka huu, huku akihoji madhara yanayoweza kujitokeza siku hiyo, hivyo akamuomba Rais kutengua amri yake ya kuzuia mikutano ya hadhara
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)