NEWS ALERT:UFAFANUZI KUHUSU TAMKO LA JESHI LA POLISI LA KUPIGA MARUFUKU MAANDAMANO NA MIKUTANO YA HADHARA YA VYAMA VYA SIASA.

Jeshi La Polisi Tanzania

Ndugu zangu waandishi wa habari.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuelimisha jamii hususani katika habari zinazosaidia kuzuia uhalifu na kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu
.

Nimewaita leo hii kutoa ufafanuzi kufuatia tafsiri na mitazamo tofauti iliyojitokeza baada ya Jeshi la Polisi kutoa tamko tarehe 07 Juni, 2016 kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, Jeshi la Polisi limeona ni vyema kurudia kutoa ufafanuzi ili wananchi wasiendelee kupotoshwa na vyama vya siasa, makundi ya watu au mtu yeyote asiye na nia njema.

Katika tamko hilo, Jeshi la Polisi tulisema bayana kuwa, nanukuu
“Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 07/06/2016 hadi hapo hali ya kiusalama itakapotengemaa.”

Hivyo, hakuna sehemu yoyote katika tamko hii iliyopiga marufuku mikutano ya kiutendaji na kiutawala ya vyama vya siasa inayofanywa kwa mujibu wa katiba na kanuni za vyama husika.


Ndiyo maana baada ya tamko la Jeshi la Polisi la tarehe 07 Juni, 2016 kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, baadhi ya vyama vimefanya na kupanga kufanya mikutano ya kiutendaji na kiutawala bila kuingiliwa ama kuzuiliwa na Jeshi la Polisi. Mifano hai ni pamoja na mkutano wa ndani wa kikazi uliofanywa na Bavicha kuongea na waandishi wa habari tarehe 03 Julai, 2016, mkutano huo ulifanyika bila kuzuiliwa, ambapo walitoa habari potofu kuwa Jeshi la Polisi wamezuia mikutano yote ya vyama hata ya kiutendaji na kiutawala kama mkutano mkuu wa chama.
(Mhasibu Mkuu wa Jeshi La Polisi Asimamishwa kazi bofya hapa)
Chama cha CUF kilitangaza kuwa kimepanga kufanya mkutano mkuu kujaza nafasi ya Mwenyekiti wao wa Taifa tarehe 21 Agosti, 2016, Jeshi la Polisi halijajitokeza kuwazuia kwani hayo siyo maandamano au mkutano wa hadhara. Pia, katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad alifanya vikao vya ndani vya chama chake huko Zanzibar, ijapokuwa mara baada ya vikao hivyo kulianza kujitokeza matukio mbalimbali ya kiuhalifu kama vile kuchoma moto mashamba, kukata mazao, mashambulizi na vitendo vya kibaguzi. Matendo haya ni uvunjifu wa sheria na jeshi la polisi limechukua hatua kwa wote waliohusika na matukio hayo.

Aidha, shughuli ya Jumuiya ya ndani ya wanafunzi wa vyuo vikuu ya CHADEMA (CHASO) iliyopangwa kufanyika Dodoma na ile ya ACT iliyopangwa kufanyika Dar es salaam ilizuiliwa kwa sababu kuu mbili:-

(i) Jumbe katika shughuli hizo zililenga kufanya uchochezi utakaopelekea uvunjifu wa amani
(ii) Shughuli zile hazikuwa mikutano ya kiutendaji au kiutawala ambayo inaandaliwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama.

Kufutia hali hiyo, pamoja na kwamba, vyama vya siasa vina utaratibu wake wa kufanya mikutano ya ndani ya kiutawala na kiutendaji, bado Jeshi la polisi kwa mujibu wa sheria lina mamlaka ya kuzuia pale inapobainika kuwa mikutano hiyo imelenga kuhamasisha uchochezi unaoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi yetu au wa eneo husika. Hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza kuwa limepiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara mpaka pale hali ya kiusalama itakapotengemaa.
(Video: Ufafanuzi kuhusu tamko la Jeshi la Polisi Kupiga Marufuku Mikutano na maandamano ya kisiasa bofya hapa)
Jeshi la Polisi nchini, linatoa wito kwa wananchi wote na vyama vya siasa kuheshimu sheria z anchi na wakati wote kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika. Aidha, kauli zozote zinazolenga kuhamasisha uchochezi hazitavumiliwa, na yeyote atakayetoa kauli hizo atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.


Imetolewa na:
NSATO MARIJANI MSSANZYA,
Kamishina wa Polisi- Oparesheni na Mafunzo,
Makao Makuu ya Polisi.
09/07/ 2016

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top