N’GOLO KANTE JINO LA CONTE KWENYE MFUPA ULIOWASHINDA MAN UTD



Inasemekana ni ngumu kutwaa taji la ligi kuu England endapo timu ikatumia 3-5-2. Luis Van Gaal alishika nafasi ya tatu kwenye Kombe la dunia kupitia 3-5-2 baadae mfumo ukageuka mfupa mgumu uliomshinda fisi alipojiunga na Man United. Kupitia mabeki watatu, viungo watano na washambuliaji wawili Man United chini ya Van Gaal ikawa timu yenye kuruhusu mabao kirahisi hatimae akaamua kuachana na mfumo huo.

Waingereza wanasema timu zote ambazo zimechukua ubingwa wa ligi kuu tangu kuanzishwa mwaka 1992, hakuna timu hata moja ambayo imewahiwa kutumia mfumo huu. Sio Arsenal, Man United, Blackburn Rovers, Man City, Chelsea au Leicester imeweza kutwaa taji na 3-5-2. Hata ile Arsenal iliyosifika kuwa na safu bora ya ulinzi chini ya Kocha Mscotishi George Graham mwishoni mwa miaka ya tisini kumbukumbu zinaonesha haikutumia mfumo wa mabeki watatu wakati wakielekea kutwaa taji.

Lakini kuna kitu cha kufurahisha kwa kocha mpya wa Chelsea, Antonio Conte. Mafanikio ya Conte ndani ya Serie A ni kupitia mfumo ambao umefeli ndani ya England. Kufeli huku yawezekana ndio sababu ya Conte kutoweka bayana jinsi Chelsea itavyocheza kwenye mechi za Ligi kuu. Kufeli na kufaulu kwa Conte tutaona punde tu ligi itapoanza kama tulivyoona kwa Luis Van Gaal ambaye wapenzi wa Man Utd walikuwa na matumaini makubwa juu yake.

Conte anatengeza timu yake kupitia dirisha la usajili na tayari amemnasa kiungo bora wa ulinzi barani Ulaya kwa msimu uliopita. Ndio ni bora sababu hata takwimu zake hususani kwenye eneo hilo yeye amefanya vizuri zaidi ya wote kwenye ligi kubwa barani Ulaya. Naongelea usajili wa N’Golo Kante kutoka Leicester City kwenda Chelsea.

Bila shaka Conte amelamba dume labda yatokee mambo mengine kwenye mpira mfano majeruhi au game imkatae pale Stamford Bridge. Kante akiwa sawa kwa msimu mzima wa ligi atakuwa muhimili mkubwa kwenye eneo la kiungo. Uwezo mkubwa wa kuzima mashambulizi kama alivyoonesha na Leicester msimu uliopita ataisaidia sana safu ya ulinzi hususani wale mabeki watatu kama Chelsea itaendelea na mfumo ambao upendwa sana na Conte.

Tengeneza taswira endapo wale mabeki wa tatu wa nyuma mbele yao kukiwa na viungo wengine wawili wa kukaba mfano Kante na Nemanja Matic au Raja Nainggolan Yule kiungo wa Belgium anayependa kunyoa mtindo wa “kiduku”. Mbele yao kuwe na Cesc Fabregas katikati, kushoto Eden Hazard na kulia Willian.

Mtu kama Kante ana uwezo wa kuwalinda kina Courtis Zouma, Garry Cahill na John Terry kwa kufanya tackling za uhahika kabla mashambulizi hayajafika kwenye eneo la hatari la Chelsea. Pia Kante sio mbaya sana kwenye kuanzisha mashambulizi ya haraka kuelekea mbele. Kumbuka tu Leicester ilivyokuwa na tabia ya kushambulia na kufunga magoli kwa staili ya mambalizi ya kushtukiza kwenye msimu uliopita.

Kupitia kina Kante upo uwezekano wa Conte kuweka rekodi mpya kuchukua ubingwa kupitia mfupa mgumu, mfumo wa 3-5-2 ambao uliowashinda Man United ya Luis Van Gaal.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top