Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson amesema hoja ya wabunge wa Ukawa kutaka aenguliwe kwenye wadhifa huo inafanyiwa kazi na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo iwapo itaridhia, itarejeshwa bungeni kupigiwa kura ambazo hata hivyo, hazitatosha kwa uchache wao.
Dk Tulia alisema hayo jana wakati akihojiwa na Tido Mhando katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Azam TV.
“Hoja ikishakuja bungeni hapo sasa huwa ni kampeni na baadaye kupigiwa kura. Kwa kuwa waliopeleka hoja ni wabunge wa upinzani, hivyo wanatakiwa kufikisha idadi fulani ambayo kiuhalisia wao kwa sasa hawana,” alisema.
Kwa karibu mwezi mzima kwenye Bunge la Bajeti, wabunge wa Ukawa walimsusia Dk Tulia na walikuwa wakitoka bungeni kila alipoingia, tayari wameanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani kwa madai kuwa hawatendei haki na anaminya demokrasia ndani ya Bunge.
Dk Tulia alisema Katiba inatambua kwamba kiongozi aliyechaguliwa anaweza kuondolewa madarakani na wale waliomchagua, hivyo wabunge wa upinzani wametumia haki yao ya msingi na kinachosubiriwa ni hoja yao kufanyiwa kazi.
“Kanuni imeweka wazi na msingi ule umejengwa kwenye Katiba kwa sababu inatambua wale waliomchagua kiongozi wasiporidhika naye wanaweza kumuondoa madarakani. Nafarijika kuona wanachukua hatua, hivyo mimi sina malumbano nao,” alisema.
Hakuna maridhiano
Dk Tulia alisema hakuna maridhiano yanayotakiwa baina yake na wabunge wa Ukawa kwa kuwa hana malumbano nao, bali kanuni na taratibu zinafuatwa kufanikisha hoja yao ya kumuondoa madarakani.
Naibu Spika huyo alisema maridhiano huwapo baina ya watu wanaolumbana na kwamba, baina yao hakutakuwa na suala hilo.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)