Mamia wafurika kununua viwanja Dodoma

MAMIA ya wananchi wameanza kupeleka maombi ya viwanja katika ofisi za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), imeelezwa.


Hali hiyo imetokea baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza nia ya Serikali kuhamia mjini hapa kwa kuwa ndiko yaliko makao makuu ya nchi.


Kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofika katika ofisi za Idara ya Ardhi katika mamlaka hiyo, Jeshi la Polisi mkoani hapa limelazimika kuimarisha ulinzi ili kukabiliana na hali hiyo.


Mmoja wa watu waliokutwa ofisini hapo na kujitambulisha kwa jina la Salum Kijuu, mkazi wa Area A, alimwambia mwandishi wa habari hizi aliyeshuhudia mamia ya watu ofisini hapo jana, kwamba alifika ofisini hapo kulipia kiwanja chake kilichopo eneo la Miganga.


“Kaka hii foleni ya watu karibia wote wanaulizia viwanja, mimi nimekuja kulipia kiwanja changu ili niweze kukimiliki kihalali kwani mambo yameshabadilika,” alisema Kijuu.


Wakati hali ikiwa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili, alisema ardhi mjini hapa itauzwa kwa bei ya kawaida ili watu wengi waweze kumiliki viwanja.


“Kwa mfano, ‘square’ mita moja ya kiwanja cha makazi itauzwa kwa Sh 5,500 hadi Sh 10,000 katika maeneo ambayo kitaalamu tunayaita ‘medium density’.


“Kwa sasa maeneo yanayouzwa ni Miganga na Mkalama yaliyopo nje kidogo ya mji wa Dodoma.


“Viwanja kwa ajili ya uwekezaji mkubwa ‘square’ mita moja itauzwa kwa Sh 13,300 na maeneo hayo kitaalamu tunayaita ‘low density’.


“Pamoja na uwepo wa mahitaji makubwa, nasema ardhi ipo ya kutosha, yaani hata kama watakuja wananchi wote wa Dar es Salaam, watapata ardhi ya kutosha.


“Narudia tena, ardhi ipo ya kutosha, hata kama watu watakuja baada ya miaka 30, wataipata kwa sababu hata Mwalimu Nyerere alipoamua Dodoma iwe makao makuu, alijua kuna ardhi ya kutosha kwa idadi yoyote ya watu,” alisema Muragili.


Akizungumzia mpangilio wa mji utakavyokuwa, alisema mji wa kiserikali utaanzia katika Kijiji cha Mtumba hadi eneo la Ikulu ndogo ya Chamwino, ambako kutakuwa na ofisi za wizara na mabalozi.


“Mji wa kibiashara, utakuwa ni eneo lote la mji wa Dodoma kwa sababu hii ramani ninayokwambia iko katika ‘master plan’ ya mwaka 2010-2030 ya kuhakikisha makao makuu ya nchi yanakuwa vizuri kuanzia kwenye barabara za kuingia na kutoka ili kusiwe na msongamano wa aina yoyote,” alisema.


Pamoja na hayo, mkurugenzi huyo alitoa angalizo kwa wanaohitaji kununua viwanja mjini Dodoma na kusema watatakiwa kupitia CDA kwa kuwa ndiko vinakopatikana.


“Viwanja tusinunue kienyeji, tufuate taratibu kwani najua watatokea wapigaji wa dili watakaowaumiza watu. Nawaombeni mje ofisini kwetu, kama mnataka viwanja mtapata tu kwa kufuata utaratibu,’’ alisema.


Naye Ofisa Uwekezaji wa CDA, Abeid Msangi, alisema wametenga maeneo maalumu ya Itega na Njendengwa kwa ajili ya kujenga mahoteli makubwa na nyumba mbalimbali za kupanga.


“Lakini kwa sasa eneo la Itega limeshajaa, ila Ndejengwa tumetenga zaidi ya ekari 1,500 kwa ajili ya uwekezaji mkubwa.


“Kuonyesha kwamba tulijipanga mapema katika eneo la uwekezaji, kule Ndejengwa miundombinu iliishafika mapema, kwani kuna maji, umeme pamoja na barabara za lami,” alisema Msangi.


Hivi karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema watazalisha umeme wa megawati 60 ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Dodoma.


Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa kujenga njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Singida.


Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, Mkoa wa Dodoma (Duwasa), David Pallangyo, ameshasema wamejipanga kuhakikisha maeneo yatakayopimwa, yanapata maji safi na salama.


Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dodoma, Bernard Chimagu, naye alishasema wamejipanga kukabiliana na ongezeko la magari.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top