Majaliwa:serikali Kuendelea Kushirikiana Na Madhehebu Yote Nchini


WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inaunga mkono dini zote nchini na kuzipa ushirikiano wa kutosha ili ziweze kufanya kazi zake vizuri.

“Dini ndiyo inayojenga msingi imara kiroho, kiimani na ndiyo inajenga maadili mema. Leo tunaposema kila mtu awe muadilifu tumegundua ili tufanikiwe lazima tuweke mazingira mazuri yatakayowezesha madhehebu yote kuabudu kwa uhuru,” alisema.


Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi Julai 14, 2016) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Malolo na Chimbila ‘B’ akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Ruangwa.


Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imegundua kuwa ili iweze kufanikiwa ni lazima ishirikian na madhehebu ya yote ili yaweze kufanya kazi zake vizuri.


“Nikiwa mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali niliamua kuunda kamati ya amani ya Taifa ambayo inajumuisha viongozi wa dini zote. Pia nimeiagiza mikoa na wilaya zote kuunda kamati za amani ili kuhakikisha umoja na maelewano miongoni mwa dini zote nchini unakuwepo,” alisema.


Alisema lengo la kamati hizo za amani ni kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na maadili mema na kutambua umuhimu wa kuimarisha amani na utulivu nchini.


Akizungumzia tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vya Nanganga, Nangumbu, Mbecha, Malolo, Mpumbe na Chimbila ‘B’ alisema Serikali inalifanyia kazi suala hilo.


Alisema tayari mtaalamu wa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi ameshawasili katika wilaya hiyo na baada ya kukamilisha utafiti huo shughuli ya uchimbaji visima itaanza.


Waziri Mkuu alisema lengo la utafiti huo ni kutaka kubaini wingi na ubora wa maji katika eneo husika hivyo aliwataka wananchi wa eneo hilo kuwa na subira wakati suala hilo likishughulikiwa.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top