Hatima ya Abdulrahman Kinana mikononi mwa Rais Magufuli..

HATIMA ya nani atakuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ipo mikonini mwa mwenyekiti mtarajiwa Rais Dk. John Magufuli, ambaye sasa yupo mbioni kukabidhiwa mikoba ya chama hicho.


Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Abdulrahman Kinana, ambaye ameshika nafasi hiyo tangu Novemba, 2012.


Jana Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema hadi sasa maandalizi yanakwenda vizuri na tayari wajumbe wataanza kuwasili mjini Dodoma mapema wiki hii, kwa ajili ya Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 23, mwaka huu.


“Suala la nani ni Katibu Mkuu litaamuliwa na mwenyekiti mpya Dk. John Magufuli, baada ya kukabidhiwa chama na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Tunataraji wajumbe 2,465 watahudhuria na hata wakipungua basi ni kidogo,” alisema


Msemaji huyo wa CCM alisema kuwa baada ya Julai 23, kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ambacho ndicho kitaamua juu ya mapendekezo ya mwenyekiti mpya kama anabadili sekretarieti au laa.


“Kwa sasa Katibu Mkuu bado ni Kinana hivyo sasa hapo ndipo kuna kitandawili ambacho kitateguliwa na mwenyewe Rais Magufuli kama ataendelea na aliyepo sasa au atakuja na mtu mwingine,” alisema Sendeka.


Alipoulizwa kuhusu kuibuka kwa kundi la watu wanaompinga Rais Magufuli, asipigiwe kura kwa ajili ya kukabidhiwa chama, alisema hakuna kitu kama hicho zaidi ya taarifa hizo kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii.


“Suala la kuwepo kwa watu kumpinga Rais Magufuli asikabidhiwe chama si geni, ingawa hadi sasa hatujaweza kumfahamu mwanachama yeote anayeendesha mpango huu.


“Mambo haya nahisi kuna kikundi cha watu kinajifurahisha katika mitandao ya kijamii hivi inawezakana vipi wajumbe walewale waliomchagua Magufuli awe mgombea wa CCM eti leo hii wageuke na kumpinga?


“… hili si kweli na si geni kama unakumbuka hata mwaka 2002 wakati mzee Benjamin Mkapa anawania uenyekiti kwa mara ya pili mambo kama haya yalijitokeza na wale waliokuwa wanatajwa walikanusha na haohao ndiyo wakawa mstari wa mbele kuhakikisha wanatafuta kura za kutosha,” alisema Sendeka.


Hata hivyo hadi sasa bado Kinana amekuwa akipewa nafasi ya kuendelea kuwa katibu mkuu ingawa mwenyewe amekuwa akitajwa na watu wake karibu kuwa anahitaji kupumzika.


Polisi wachimba mkwara
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo mkoani hapa Mayala Towo, alisema polisi wamejipanga kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kisima cha amani wakati wote na baada ya Mkutano Mkuu wa CCM.


“Amani itakuwepo wana Dodoma na Watanzania wasiwe na wasiwasi ukija na nia mbaya tutakachokufanya utawasimulia wenzako kwani kwetu amani ni wajibu wetu,” alisema Mayala.


Alitoa angalizo kwa wale watakaopokea na kuwaweka wageni katika nyumba zao ambao lengo lao ni kufanya fujo kuwa jeshi hilo litawachukulia hatua kali za kisheria.


“Usiwe sehemu ya tatizo, kama unampokea mtu na kumweka kwako ili aje afanye vurugu wa kwanza kuchukuliwa hatua utakuwa wewe mwenye nyumba,” alisema.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top