Wabunge wa vyama vinavyounda Ukawa jana walisusia futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwa ni mwendelezo wa hatua za kususia shughuli zote zinazoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Riziki Ng’wale, alisema wamechukua hatua hiyo kutokana na Dk Tulia kuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo.
“Dk Tulia ndiye mgeni rasmi katika shughuli hiyo ya kufuturisha na sisi tumeamua kuwa hatutashiriki shughuli yoyote inayoongozwa naye,”alisema muda mfupi baada ya kutoka katika kikao cha wabunge wa kambi hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema wamekubaliana wabunge wote wa kambi ya upinzani waliofunga watakwenda kufuturu majumbani kwao.
“Tumekubaliana hatutakwenda kufuturu bungeni na kila mbunge atakwenda kufuturu nyumbani kwake,” alisema.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha wapinzani kilichoketi chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia.
Futari hiyo ilitangazwa na Dk Tulia tangu juzi na kusisitizwa jana baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa mchana kuwa ingefanyika kwenye viwanja vya Bunge ambako wabunge wote walialikwa.
Kwa siku zaidi ya 10 sasa, wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Dk Tulia kwa sababu hawana imani naye.
Hali hiyo imefanya bajeti kuu kwa ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 kuchangiwa na wabunge wa CCM tu baada ya Dk Tulia kuongoza vikao kila siku, akiingia asubuhi na jioni.