Wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitengua uamuzi wake wa kung’atuka kwenye wadhifa huo na kuomba kurejea, viongozi wa juu wa chama hicho wamepinga hatua hiyo wakisema katiba yao hairuhusu na kwamba anakwenda kukiua chama.
Kauli za viongozi hao, zimekuja muda mfupi baada ya Profesa Lipumba kutangaza nia hiyo jana kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni huku akibainisha kuwa amefanya hivyo baada ya kuombwa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Lipumba hawezi kuwa na nia njema ya kukijenga chama hicho endapo atarudishwa kwenye nafasi aliyoikataa.
“Anataka kuja kukiharibu chama,” alisema Mazrui. Alifafanua kuwa tayari chama hicho kimefanya mambo mengi bila Lipumba ambaye alikuwa anaona kila kinachoendelea, hivyo alichokisema hakina mashiko kwani CUF ilisharidhia kuitisha mkutano wa uchaguzi kujaza hiyo.
Akieleza sababu alizozitoa mwenyekiti huyo, Mazrui alisema haoni chochote cha maana. “Sababu zilizomuondoa zingalipo. Kinachomrudisha ni nini?” alihoji naibu katibu mkuu huyo.
Alisisitiza kuwa Wazanzibari wanaendelea na mchakato wa kuidai haki yao iliyoporwa Oktoba 25 na hawana nafasi ya kushughulika na masuala yasiyokuwa na tija kwao, hivyo haoni kama kuna sababu ya kumjadili Lipumba na nafasi yake badala ya kuendelea pale walipo.
“CCM wanaona kinachoendelea, hivyo wameona wamtumie Lipumba kuja kuharibu mipango yetu. Hatuna muda wa kumjadili.Tunataka haki iliyoporwa,” alisisitiza.
Msimamo wa Mazrui haukutofautiana sana na ule wa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima aliyebainisha kuwa amesikia taarifa za kurudi kwa Profesa Lipumba, lakini haoni uwezekano huo.
“Katiba hairuhusu hilo.Hakuna kifungu kinachotoa nafasi kwa kiongozi aliyejiuzulu kurudi kwenye nafasi yake pindi atakapotaka kufanya hivyo,”alisema Taslima.
Aliielezea Ibara ya 117 (2) iliyotumiwa na Profesa huyo kuandika barua ya kutengua uamuzi wake, kuwa inatoa tafsiri zaidi ya moja hivyo kuwapo haja ya viongozi kukutana na kujadili suala hilo kabla ya kutoa maamuzi.
Kwa kuwa hakuwapo kwenye mkutano huo, Taslima alisema: “Tunahitaji kukutana haraka na kujadili. Tutafanya mkutano wetu na tutavijulisha vyombo vya habari ndani ya wiki hii.”
Taslima alisema kipindi alichoongoza kilikuwa na changamoto nyingi ambazo ni tofauti na sasa, hivyo haoni haja ya mtu mwingine kuja wakati mambo yametulia. Chama hicho kilipanga kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo Agosti mwaka huu.
Baada ya kung’atuka kwa Lipumba, Taslima alichukua mikoba yake na kukivusha chama hicho kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, pamoja na ule wa Zanzibar ambao uliahirishwa na chama hicho kususia marudio yake Machi 20 mwaka huu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya alisema upo uwezekano wa Lipumba kurudi kwenye nafasi yake kwasababu mpaka sasa haijazibwa.
“Mwenyekiti huchaguliwa au kutenguliwa na halmashauri kuu. Haikupitisha kujizulu. Barua ya kujiuzulu itaenda pamoja na hii ya kutengua uamuzi wa awali,” alisema Kambaya.
Kauli ya Lipumba
Awali, Profesa Lipumba alisema mara kadhaa amekutana na viongozi wa dini na chama pamoja na wanachama wa CUF na wote walikuwa na ujumbe mmoja tu…’rudi tukijenge chama.’
Profesa Lipumba hakushiriki mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao kwa upande wa Zanzibar, kutokana na hitilafu zilizojitokeza ulifutwa na kurejewa Machi 20 mwaka huu huku chama hicho kikiwa kimesusia marudio hayo.
Pamoja na hayo yote, Lipumba alisema ametafakari sana juu ya hali ya kisiasa Zanzibar na kuona umuhimu wa kutoa ushirikiano ili mambo yaende kwa manufaa ya taifa.
“Ni lazima nchi iendeshwe kwa misingi ya demokrasia ambayo itapatikana kwa umoja wetu.Nimerudi kushirikiana na wenzangu kutimiza malengo hayo ili kuchangia maendeleo ya Tanzania,” alisema Profesa Lipumba.
Lipumba aliachana na uongozi wa chama hicho, Agosti 8, mwaka jana, siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa kukubaliana kumsimamisha Edward Lowassa.
Alimuandikia barua Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad kuwa hakubaliani na uamuzi wa chama chake kuridhia makada waliohama Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Lowassa, kupewa fursa ya kugombea nafasi za uongozi.
Baada ya kukatwa kwenye mchujo wa ndani ya CCM, Lowassa akiwa na makada kadhaa wa chama hicho akiwamo aliyewahi kuwa waziri mkuu, Frederick Sumaye, alihamia Chadema ambako alipewa fursa ya kupeperusha bendera ya chama hicho kilichomo ndani ya Ukawa.
Lipumba hakukubaliana na hilo, alikaa pembeni na kuachia ngazi ingawa alishiriki tukio la kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa.
Jana, wakati anatangaza kufanya mabadiliko ya kile alichokiamua miezi 10 iliyopita, hakuruhusu maswali, ila alifafanua kile kitakachofuata baada ya kuwasilisha ombi hilo, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho:“Katibu Mkuu anashauriana na wanasheria kabla suala langu halijapelekwa kwenye halmashauri kuu kama katiba inavyosema,”alisema Profesa Lipumba.