Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya ndoto za Gerson Ngassalah (27) mkazi wa Kalobe jijini Mbeya za kufurahia maisha baada ya kuachana na ukapera kuzimwa ghafla alfajiri ya Jumatano iliyopita katika ajali iliyosababisha kupoteza uhai wake papo hapo, siku moja kabla ya harusi yake.
Gerson alipata ajali hiyo katika maeneo ya Makambako akiwa njiani kurejea jijini Mbeya akitokea Dar es Salaam alikokwenda kwenye send-off ya mchumba wake, Felister Ngowi iliyofanyika Jumatatu katika maeneo ya Sinza.
Harusi ya wawili hao ilitarajiwa kufanyika Alhamisi jijini Mbeya lakini Gerson hakuifikia akimuacha mchumba wake akiwa mjamzito.
Badala ya siku hiyo kuwa ya furaha, ikawa ndiyo ya mazishi ya kijana huyo.
Akizungumza nyumbani kwa wazazi wao, Emmanuel Ngassalah ambaye ni kaka mkubwa wa marehemu alisema Jumatatu ya Juni 20, marehemu akiambatana na ndugu zao wengine walihudhuria sherehe ya kumuaga mchumba wake na baada ya shughuli hiyo walitawanyika kurudi nyumbani kwa ajili ya kujiandaa na safari ya kurejea Mbeya.
“Kesho yake (Jumanne) mdogo wangu pamoja na ndugu wengine walianza safari saa moja jioni kuja Mbeya kuwahi harusi na mchumba wake alishakatiwa tiketi ya ndege na mchumba wake na alisafiri Jumatano asubuhi akiwa na mama yake mdogo,” alisema Emmanuel.
Alisema katika msafara wa bwana harusi walikuwa na magari mawili, Gerson na ndugu zake watano na jingine ambalo lilibeba watu sita lililokuwa mbele.
Emmanuel alisema gari la mbele liliwaacha umbali wa kilomita 100 hivi na walipofika njia panda ya Ilembula (Njombe) alfajiri ya saa kumi na moja, mmoja wao alimpigia simu na dada yetu Aines, akiwajulisha kwamba wamepata ajali, gari lao limepinduka eneo la Chimba dawa – Makambako, hivyo warudi haraka.
Alisema walipofika pale walimkuta Gerson akiwa amepoteza fahamu, mwingine akiwa amevunjika mguu lakini watatu wakiwa salama, hivyo kumpeleka Hospitali ya Ilembula lakini walipofika madaktari waliwaambia ndugu yao amepoteza maisha.
“Basi hapo kukawa hakuna namna nyingine, ukafanyika utaratibu wa kubeba mwili wa marehemu hadi Mbeya.
Alisema asubuhi hiyo saa mbili, mchumba wa marehemu naye alifika akiwa na mama yake mdogo na walikwenda moja kwa moja hotelini walikopanga kufikia na Gerson.
Mchumba azimia
Emmanuel alisema baada ya mchumba wake kupata taarifa kuwa mumewe mtarajiwa hayupo tena duniani, alilia kwa uchungu na wakati wa kuweka mashada ya maua makaburini, aliishiwa nguvu na kuanguka na walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya ambako ilibainika kuwa ameishiwa maji. Baada ya matibabu, aliruhusiwa kutoka Ijumaa iliyopita.
“Kwa sasa hutaweza kumuona wala kuzungumza naye, huyu binti hayupo vizuri kabisa. Tunajitahidi kumfanyia ushauri ili aweze kurudi katika hali yake japo itamchukua muda kidogo kuwa sawa,” alisema Emmanuel.
Baba Mdogo wa Felister, Jonathan Ngowi alisema wakiwa safarini kwenda Mbeya kwa ajili ya harusi na mtoto wao walipokea simu kutoka kwa binamu yake kwamba mambo yameharibika kwani mkwe wao ameoteza maisha katika ajali.
“Mipango ya Mola ikageuza furaha kuwa msiba mzito kwetu sote. Hatuna namna nyingine tunamuachia Mola mwenyewe,” alisema Ngowi na kuongeza: “Kwenye gari tulikuwa watano, nilipopokea simu ile kutoka kwa binamu yangu, akawa ananiuliza vitu ambavyo sikumuelewa kabisa na ghafla akakata simu, lakini mimi nikampigia tena bado akawa anababaika kusema, mwisho nikamwambia niambie kuna tatizo gani?
“Baadaye akaniambia, bwana mpo safarini lakini huko mnakokwenda siyo salama kabisa, mkwe wenu amepata ajali na amefariki. Hapo nikakaa zaidi ya dakika 10 bila kusema chochote, baadaye mke wangu akaniuliza ‘kulikoni mbona upo kimya tangu umalize kuongea na simu?’”
Alisema alichelewa kidogo kumweleza mke wake kwa kuwa nyuma ya gari hilo walikuwa wamekaa wazazi wa Felister, lakini hakuwa na namna yoyote ile ikambidi amnong’oneze tu mkewe, ndipo wakaambizana kukaa kimya bila ya kuwaambia hadi watakapofika Mbeya.
“Lakini ghafla taarifa zikaenea kwenye mitandao ya kijamii (WhatsApp), kuna mtu alipopata taarifa hizo akaamua kuzirusha, ndipo akazipata ndugu yao mwingine ambaye alimpigia baba wa Felister kumuuliza juu ya taarifa hizo.”
Alisema baada ya kuona hivyo, ikabidi amuweke wazi kwamba ni kweli tukio hilo lipo na ameshapewa taarifa na binamu yake aliyekuwa mshenga, lakini akawaeleza kwamba hawana namna nyingine ni lazima wafike Mbeya kwenye msiba badala ya harusi.
Like page yetu ya facebook upate habari kwa urahisi na haraka zaidi BOFYA HAPA
HABARI KUU LEO BOFYA HAPA