Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuongeza uelewa kuhusu ualbino yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama cha Watu Wenye Ualbino Nchini (Tanzania Albinism Society) Nemes Temba ameeleza kuwa kupitia maadhimisho hayo jamii itapata fursa ya kupewa elimu muhimu kuhusu ualbino ili kuondoka na dhana potofu hususani ushirikina.
“Maadhimisho haya ambayo yataanza Juni 11 hadi Juni 13, 2016 yatasindikizwa na mambo mbalimbali ikiwemo huduma za afya hususani uchunguzi na matibabu ya saratani ya ngozi pamoja na nasaha za viongozi na mabalozi, utambulisho wa Miss Albino Tanzania na uzinduzi wa kamusi ya ulemavu,” alisema Temba.
Temba aliendelea kuainisha kwamba siku hiyo itawapa fursa watoto wenye ualbino waishio kwenye vituo mbalimbali nchini kutembelea mji wa Bagamoyo kujionea mambo mbalimbali chini ya ufadhili wa shirika la UNICEF.
Aidha Mwenyekiti huyo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwapa vipaumbele watu wenye ulemavu akiwemo Dkt. Abdallah Possi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Kazi na Watu Wenye Ulemavu hii inadhihirisha kuwa ulemavu si hoja bali utendaji kazi ndio kitu umuhimu.