Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza kutoa vitambulisho vya Taifa vyenye saini ya mwenye kitambulisho kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Mamlaka hiyo Bi. Rose Mdami wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Mdami alisema kuwa lengo la Mamlaka hiyo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata vitambulisho vya Taifa ambapo katika hatua ya kwanza mamlaka hiyo inachakata taarifa za wananchi walizotoa wakati wa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Utoaji wa vitambulisho hivi vyenye saini ya mwombaji utasaidia kuwatambua wahusika pale wanapohitaji huduma mbalimbali za kijamii.
“Upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa utasaidia Serikali kuondokana na tatizo la Watumishi hewa kwa kuwa mfumo wetu utaunganishwa na mifumo mingine inayosimamia utumishi wa umma” alisisitiza Mdami.
Utoaji huo wa vitambulisho utaanza kwa kutoa namba za utambulisho kwa wananchi ili zisaidie katika upatikanaji wa huduma mbalimbali wakati mchakato wa kuzalisha vitambulisho hivyo ukiendelea.
Mdami alifafanua kuwa baada ya kuchakata taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi zitarudishwa kwenye mitaa na vijiji husika kwa ajili ya uhakiki wa taarifa hizo.
Lengo la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba mwaka huu wananchi wote wawe wamepatiwa namba ya utambulisho .