NI mnazi wa Simba, lakini mzee Ally Samatta kesho Jumanne atakuwa shabiki wa Yanga wakati mabingwa hao wa Bara watakapoikaribisha TP Mazembe
.Unajua ni kwanini asiishabikie Mazembe ambayo imemtoa mwanaye, Mbwana Samatta, na kumfanya naye anufaike kimaisha na mafanikio ya kijana wake huyo ambaye sasa anakipiga katika klabu ya Genk ya Ubelgiji?
Kuna mengi yanayomfanya Mzee Samatta awe ni hasimu wa Yanga. Mwanaye alichezea Simba kabla ya kusajiliwa na Mazembe na yeye mwenyewe pia ni mwanandinga wa zamani wa Simba enzi hizi ikiitwa Sunderland.
Lakini licha ya yeye na mwanae kuwa na mapenzi na timu hiyo kongwe ya mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, anasema ni lazima aishabikie Yanga kutokana na kuwa ndiyo timu inayoweza kuibeba Simba kushiriki kwenye michuano ya kimataifa mwakani.
Unajua mzee kapiga hesabu gani? Ameziangalia kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kuzielewa na kugundua kuwa kama Yanga itatinga nusu-fainali inaweza kuibeba Simba ishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani baada ya kuikosa kwa miaka minne.
Pamoja na kukubali kiroho safi kuishabikia Yanga, amesema kuwa anawaona wachezaji Deogratius Munishi ‘Dida’ na Godfrey Mwashiuya kuwa ndiyo wazawa pekee wanaoweza kufuata nyayo za Mbwana.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, alionwa na Mazembe 2011 kwenye mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Simba na miamba hao wa Afrika kushinda 3-2 jijini Dar es Salaam na kisha 3-1 kwenye mchezo wa marudiano kule Lubumbashi, DRC. Simba ilisonga mbele, hata hivyo, kwa ushindi wa mezani.
Yafuatayo ni mambo mbalimbali ambayo mzee Ally Samatta ameyaeleza kuelekea mechi ya Yanga dhidi ya TP Mazembe huku akigusia sababu Mbwana kufanikiwa.
Aishabikia Yanga
Mzee Samatta anasema, “Kwakuwa ni Yanga inacheza na ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania nitawashabikia kwa kuwa wanaitangaza nchi. Mimi zamani nilikuwa mchezaji wa Sunderland (sasa Simba) na sasa shabiki mkubwa, lakini nataka ishinde iende nusu-fainali ili msimu ujao kuwe na timu mbili zitakazoliwakilisha taifa la Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
“Kama wakienda nusu-fainali basi na Simba nayo itakuwa kwenye nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya kimataifa. Naamini Yanga itaitengenezea njia klabu yetu ya Simba,” anasema.
Mafanikio ya Yanga kuyanufaisha Simba?
CAF ina utaratibu wa kuyapa mashirikisho bora au yaliyowakilishwa vizuri nafasi ya kuwa na timu ya pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho. Hapa tunazungumzia ‘CAF 5-Year Ranking’ ambayo inatoa fursa kutokana na jinsi timu shiriki ilivyojikusanyia pointi.
Kwa mujibu wa vigezo vya viwango vya CAF, kama Yanga ikitinga nusu-fainali na kutolewa kwenye hatua hiyo itakuwa imejikusanyia pointi mbili na kama itatwaa taji itakuwa na pointi nne wakati ikipoteza mechi itatwaa pointi tatu ambapo ni wazi kuwa Tanzania itaweza kuwakilishwa na timu nzuri.
Kwa mantiki hiyo kwakuwa Yanga tayari imeshajihakikishia kushiriki michuano ya Klabu Bingwa mwakani baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ulioisha na Azam ikapata nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho basi Simba ambayo ndiyo anayezifuata timu hizo kwenye ligi atapewa fursa ya kushiriki kama timu ya pili kwenye michuano hiyo ambayo Yanga inapambana kuona wanafanikiwa.
Utaratibu huo umekuwa ukifanywa na CAF tangu 2011 kwa mashirikisho ambayo timu zao zitakuwa zimetinga nafasi nusu-fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Pia vigezo hivyo vinatumika kwenye mashirikisho ambayo timu zao zinafanya vyema kwenye Klabu Bingwa Afrika.
Yanga ikicheza usiku itafungwa
Samatta ambaye ni baba mzazi wa kiungo mshambuliaji wa Mgambo JKT, Mohamed Samatta, anasema kuwa kitaalamu anaamini kuwa Yanga itashinda kama itacheza mchana vinginevyo wakicheza usiku watajikuta wanafungwa kiulaini.
Anasema, “Yanga wakicheza usiku watafungwa kwasababu TP Mazembe ni wazoefu wa kucheza mechi za usiku. Pia kama kigezo ni cha kuwaacha watu wenye imani ya Kiislamu wafuturu kisha kwenda kuona mechi, ni bora waache hivyo na kucheza mapema kisha kwenda kufuturu baada ya mechi.
“Mimi ni Muislamu kiimani, hainijii akilini mechi ingoje watu wafuturu wakati wachezaji kwa wakati huo hawataweza kufuturu kwasababu kiafya hawawezi kula chakula na hapo hapo kuingia uwanjani kucheza,” alisema mzee huyo huku akibainisha dawa ya kuishinda TP Mazembe kuwa ni kucheza kuanzia saa tisa au 10 alasiri siku hiyo. Hata hivyo, mechi hiyo imeshaamuliwa itachezwa saa 10:00 jioni.
Awapeleka nje Dida, Mwashiuya
Mzee Samatta amesema mbali na kufanikiwa kwa Mbwana ambaye yuko Genk, alikuwa amemtabiria mafanikio kiungo Farid Musa aliyekuwa akiichezea Azam kuwa angeweza kucheza soka la kulipwa na sasa anamtabiria kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ na winga Godfrey Mwashiuya.
Anasema, “Kwa jinsi nilipomuona Farid Musa mara ya kwanza niliwauliza watu mbona anacheza kama mimi enzi hizo niko Sunderland; mbio na ujanja ujanja kama wangu? Nilipouliza jina lake, nikaambiwa ni Farid na ndipo niliposema atafika mbali na kweli amefika mbali kwani hivi sasa anajiunga na klabu ya Tenerife ya nchini Hispania.
Kuhusu mafanikio ya Dida na Mwashiuya, mzee Samatta anasema, “Nadhani Mwashiuya ndiye mchezaji bora kwenye kikosi cha Yanga, kama angekuwa hadharauliki na anapewa nafsi mara kwa mara bila shaka angekuwa na msaada mkubwa sana kwenye timu.
“Kama atacheza dakika zote dhidi ya TP Mazembe ninamuona akienda kusajiliwa huko au kwenye timu nyingine ambayo itampeleka mbali kisoka,” anaeleza.
Kwa upande wa Dida anasema kuwa ndiye mchezaji mzoefu pekee wa Kitanzania anayeweza kusajiliwa TP Mazembe, huku akiwataja Wazimbabwe Donald Ngoma na Thabani Kamusoko kuwa miongoni mwa wachezaji watakaohitajika sokoni baada ya michuano kuisha.
“Wachezaji wazoefu wenye nafasi zaidi ni wa kigeni ambao ni Ngoma na Kamusoko, lakini kwa upande wa wazawa namwona Dida akienda kushirikiana na kipa wa Mazembe mkongwe Robert Kidiaba.
“Dida amekuwa akiiokoa timu, lakini pia amekuwa mwepesi na mwenye maamuzi ya haraka. Bila shaka amekuwa na msaada mkubwa kwa Yanga kila wakati timu hiyo inapokuwa imezidiwa,” anafafua Samatta ambaye pia ni kocha mwenye leseni ‘B’.
Amtabiria Ulimwengu kuchemka
Mzee Samatta anaamini kwamba mshambuliaji Mtanzania Thomas Ulimwengu huenda akashindwa kucheza vizuri dhidi ya Yanga kutokana na kujulikana na wachezaji wengi wa timu ya Yanga ambao wengi wao ndiyo wanaounda naye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Anasema, “Ulimwengu ana wakati mgumu sana, atakabwa na watu wanaomfahamu na naamini kuwa kila kona atakutana na vizuizi kwani wengi atakaocheza dhidi yao wanafahamu staili yake ya uchezaji.”
Kufika alipo Samatta kunahitaji nini?
Baba huyo wa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka la ndani, anasema, “Mbwana amefika alipo kutokana na nidhamu. Licha ya kuwa mimi nilikuwa polisi na mama yake alikuwa polisi, kwake ilikuwa kitu muhimu na alifanya kila jambo kwa nidhamu ya juu na hicho ndicho kinachomsaidia sasa. Kama wachezaji Yanga wanataka kufanikiwa kama Mbwana wanapaswa kucheza kwa nidhamu ya juu dhidi ya TP Mazembe na hata timu nyingine watakazocheza nazo.
“Wachezaji hawapaswi kupata kadi za njano kirahisi, hawapaswi kucheza vizuri na kuwa na sifa ya kucheza rafu. Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wanapaswa kufahamu kuwa mpira si nguvu bila maarifa. Hawapaswi kucheza kwa nguvu na kwa hasira huku wakicheza rafu mbaya,” anasema.
Anachokifanya Samatta kuendeleza soka Tanzania?
Baba huyo anaenda mbali na kusema kuwa mwanaye ana mipango mbalimbali kama kuanzisha ‘academy’ za soka, lakini la haraka ambalo linawatengenezea Watanzania fursa ni zile nafasi mbili za wachezaji kila mwaka kujiunga na Genk.
Anasema, “Mbwana amepanga mambo mengi kwa faida ya Watanzania. Mbali na miradi ya soka ambayo anataka kuianzisha, kupitia yeye klabu yake imekubali kuchukua wachezaji wawili vijana kila mwaka kwa lengo la kuwaingiza kwenye ‘academy’ yao na kisha kwenye timu ya wakubwa.
Anasema, “Mbwana aliniambia alikuwa akiumia pale wanapomuuliza Tanzania ni wapi? Pia mbona haijulikani kisoka? Ingawa alikuwa akiwajibu, ‘mimi ni mmoja wa Watanzania niliyebahatika kufika nilipo sasa na kwamba kuna Watanzania wengi na wenye uwezo kuliko mimi’.”
Anachokikumbuka, TP Mazembe ilipokuja mara ya mwisho Tanzania
Mara ya mwisho TP Mazembe kuja Tanzania kucheza dhidi ya Simba si matokeo ambayo yalimshangaza bali anadai mashabiki wa Simba ndiyo waliomshangaza zaidi pale walipomtengeneza shujaa kwa kumtoa benchi na kumtengenezea nafasi ya Ulaya.
Anasema, “Mashabiki walimshinikiza kocha Patrick Phiri kumwingiza Mbwana baada ya kuona hali si nzuri, licha ya kwamba kocha hakuelewa huku kelele zikimwandama, aliona isiwe shida na ndipo alipomuingiza.
“Ni kama vile kocha hakumuamini, lakini mashabiki walimuamini mwanangu kiasi kwamba alipoingia akathibitisha ubora wake. Kiukweli hilo lilinipa faraja kwani licha ya Simba kupoteza kwa bao 3-2, alifunga bao na pia alionyesha uwezo dhidi ya mabeki wa kimataifa wa timu hiyo.”
Kufungwa jela kwa Katumbi
Baada ya Rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi, kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu (miezi 36) jela na kutakiwa kulipa faini ya dola milioni 6 (Sh. bilioni 12.9), Mzee Samatta anasema amesikitishwa sana na tukio hilo kwani kifungo cha bilionea huyo kitapunguza ukuaji wa wachezaji wa soka Afrika Mashariki na Kati.
Anasema, “Binafsi nimeumia sana, alikuwa na mchango mkubwa. Naamini kuwa kifungo chake hakitaathiri chochote na hata hivyo wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kujituma kuhakikisha wanashinda kila mchezo kama heshima kwa tajiri huyo.
“Wachezaji wafungie macho na wacheze kwa kushinda kwani Katumbi ni kipenzi cha wote. Mfano alimpenda sana Mbwana kipindi chote akiwa Mazembe.”
Mwandishi Lasteck Alfred, wa makala hii ni Mwandishi na mchambuzi wa michezo kwenye gazeti la michezo la LETE RAHA
Uingereza yatolewa michuano ya EURO 2016 Bofya hapa
Video: MESSI AKOSA PENATI NA KUISHUHUDIA CHILE IKITWAA UBINGWA COPA AMERICA bofya hapa
Breaking news: Rais Magufuli ateua Wakuu wa Wilaya na kufanya mabadiliko kidogo ya wakuu wa mikoa bofya hapa
Like page yetu ya facebook upate habari kwa urahisi na haraka zaidi BOFYA HAPA
HABARI KUU LEO BOFYA HAPA