MIAKA 10 NA THEO WALCOTT, TUMPE MKONO GANI?

Kuna kijiwe kimoja mtandaoni huwa tunakutana mashabiki wa Arsenal kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kubadilishana mawazo kuhusu timu yetu. Moja kati ya mijadala iliyonivutia hivi karibuni ni mustakabali wa Theo Walcott. Nilishtuka kugundua kumbe wana Arsenal wengi wamemchoka Walcott. Wanamtazama kwa aibu tu kwa sababu ndiye mchezaji mwenyeji zaidi ya wengine kikosini kwa sasa na unaweza kusema ameibeba nembo ya Arsenal kwa sababu hakuwahi kuonekana kokote akiwa ni mchezaji mkubwa zaidi ya Arsenal.

Mimi binafsi nina imani kubwa sana yeye pindi awapo na afya njema. Naelewa juu ya uwezo wake mkubwa wa kubadili matokeo, Naelewa juu ya ushawishi alionao kwa wachezaji wengine na mashabiki lakini kuna ukweli kuhusu yeye ambao unaanza kunipa shida sasa. Nashindwa kuchagua mkono wa kumpa msimu ujao, nimpe wa karibu au wa kwaheri? Zipo tetesi zinamhusisha na uhamisho wa kwenda West Ham UTD.

Najiuliza sijui Wast Ham wamevutiwa na Walcott kama nani? Je ni kama winga au ni kama mshambuliaji kama ambavyo Theo mwenyewe amekua akiamini? Naukumbuka vizuri mwaka 2013 wakati Walcott akigomea mkataba mpya mpaka ahakikishiwe nafasi ya kucheza kama mshambuliaji. Aligoma katakata kwamba kuchelewa kwakebkusaini mkataba hakukuhusiana na suala ya fedha, bali haja ya moyo wake kucheza kama mshambuliaji.

Arsene Wenger alijikuta akiburuzwa na Walcott mpaka ndani ya miezi 6 ya mwisho wa mkataba wake. Hii ina maana kwamba angeweza hata kuzungumza na klabu nyingine yoyote. Asante sana kwake kwa kubaki mwaminifu kwa Arsenal.

Wakati ule siyo sawa na wakati huu. Kipindi hicho hatukua na Mesut Özil, hatukua na Alexis Sanchez. Nakumbuka staa wa timu alikua ni Santi Cazorla. Tulikua na Lucas Podolski ambaye alikua akiandamwa na majeraha, na Walcott alikua ni staa mkubwa kabisa klabuni, haikua rahisi kumuacha nje ya kikosi.

Nakumbuka sisi mashabiki tulivyompigia kocha Arsene Wenger kelele nyingi yukimtaka ampe Walcott nafasi ya kucheza kama mshambuliaji kama anavyotaka, na si winga. Wenger akafanya hivyo mara kadhaa, na wote tukashuhudia na kuridhika kwamba Walcott si mshambuliaji mzuri kama jinsi alivyo winga mzuri.

Pamoja na hayo, bado Walcott aliendelea kupata nafasi mara kadhaa, na mpaka sasa tukielekea kuuanza msimu wa nne tangu aje juu kuhusu nafasi yake, bado sioni hata dalili kama anaelekea kuitimiza hiyo ndoto. Labda majeruhi yamemtatiza, inaweza kuwa bahati mbaya sana.

Naiita bahati mbaya kwa sababu sasa hata kule pembeni ambako amekua akicheza vizuri, ameanza kuipoteza nafasi yake taratibu. Pamoja na kua na Joel Campbell na Alex-Oxlade Chamberlain ambao wana uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya winga wa kulia, bado Arsene Wenger ameonesha yu tayari hata kuwatumia Aaron Ramsey au Danny Welbeck kwenye nafasi hiyo. Taarifa zinasema Arsene Wenger alifanya mazungumzo na Theo mwishoni mwa msimu uliopita kuhusu mustakabali wake klabuni na makubaliano yakawa ni Walcott kuendelea kupigania nafasi yake.



Sasa sijui ni nafasi ipi kiwanjani, kuwa mshambuliaji wa mwisho kama akina Giroud, au anaendelea kutetea nafasi yake ya Wing? Hapa ndipo ninapopata swali kama Theo bado ana nafasi baada ya miaka 10 mizuri kwenye maisha yetu? Unamwona wapi Theo msimu ujao? Napaswa nimuulize kama bado ana ndoto ya kucheza kama mshambuliaji, kama bado anayo nitajua nimpe mkono gani.

Sitamani kumwona Walcott kwenye timu nyingine, natamani kuona akiendelea kuiwakilisha Arsenal. Lakini bado napata shaka na mtazamo wa Arsene Wenger juu yake, je bado anamtazama kama silaha zake muhimu? au anajiandaa kumfanya silaha ya akiba? Kutoka kuikataa nafasi aliyokwisha kujihakikishia mpaka kulazimika kuipigania mbele ya wadogo zake akina Joel Campbell ni hatua ngumu sana kuzikubali.

Na hapo ndipo ninapokosa mkono wa kumpa Theo. Moyo unaniambia Theo ni Arsenal, hapaswi kwenda popote kwa kua ni mzoefu na ni mtoto wa nyumbani lakini akili inaniambia tofauti hasa nikiikumbuka ndoto yake ambayo ametumia miaka 10 kushindwa kuifikia. ya kucheza kama mshambuliaji. 
Credit:Dauda
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top