MKURUGENZI wa Taasisi ya Tanzania na Maendeleo, Khamis Mgeja, amesema Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, anapaswa kuwa mtuhumiwa wa kwanza kupandishwa kizimbani katika mahakama ya mafisadi inayotarajiwa kuanzishwa Julai mwaka huu.
Amesema kiongozi huyo ndiye alihusika na kuisababishia hasara Serikali ikiwamo kuota mizizi ya ufisadi serikalini.
Mgeja amesema pia kuwa Rais Dk. John Magufuli, anapaswa kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya haraka katika baadhi ya sheria zinazowalinda viongozi kama njia ya kuondoa mfumo unaokumbatia wahalifu.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema Rais Magufuli akiamua kutenda haki katika kuwawajibisha mafisadi na wahujumu uchumi anapaswa kuanza na Rais Mkapa.
“Juzi, Mkapa tumemsikia kwenye mdahalo anaomba radhi, angekuwa muungwana angeenda mahakamani kwa makosa aliyowatendea watanzania, tunamuomba rais Magufuli aanze kumshughulikia Mkapa kupitia mahakama ya mafisadi na wahujumu uchumi aimbie dunia makosa aliyoyafanya.
“Mkapa ni jipu ila limekaa pabaya ikiwezekana rais asaidiwe,” alisema Mgeja.
Mgeja alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Alisema Rais mstaafu Mkapa ndiyo chanzo cha nchi kuwa maskini kwa kuwa aliuza rasilimali kwa bei ya kutupwa na kuruhusu ubinafsishwaji holela nchini.
“Utetezi anaoendelea kuutoa kwa wananchi majukwaani baada ya kutoka madarakani haujitoshelezi kwa kuwa makosa aliyoyafanya ni mazito, angekuwa muungwana angeenda mahakamani kutuomba radhi,” alisema Mgeja.
Alisema taasisi hiyo haimani kama Mkapa alifanya mambo hayo kwa bahati mbaya kwa kuwa alikuwa akitoa uamuzi kupitia Ikulu ambayo ni taasisi yenye wataalamu ambao wangeweza kumshauri vizuri au hata kumzuia.
“NBC kaiuza kwa Sh bilioni 16 wakati ilikuwa na mali ya zaidi ya Sh bilioni 100 … wakati anatoa uamuzi huo alikuwa mzima au alikuwa amejitwanga (kulewa) kwa sababu ni mwanachama mzuri wa hiyo kitu,”alisema Mgeja.
Akizungumzia uamuzi wa aliyekuwa mmoja wa wanachama wa Chadema, Goodluck ole Medeye kuhamia UDP, alisema mpaka sasa anaona Chadema ndiyo chama pekee cha upinzani ambacho kina nguvu ya kuondoa CCM katika dola.
Habari Kuu Leo Bofya hapa