Maana ya Saumu katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani

Maana ya Saumu;
Maana ya saumu kilugha ni kujizuia na chochote.

Maana ya saumu kisharia;
Ni kujizuia na yote yanayofunguza kuanzia kuchomoza kwa al fajiri ya kweli mpaka kuzama kwa jua Magharibi, pamoja na kuwa na nia na kujua kuwa umo katika saumu.

Uchambuzi wa Maana:
Kujizuia:-
Vinatolewa kwa neno hili vitu ambavyo huwezi kujizuia navyo kama vile kuingiwa na nzi katika koo au kuingiwa na vumbi mpaka rohoni bila hiari; haya hayavunji saumu kwani kujilinda nayo ni kugumu na Mwenyezi Mungu anasema katika surati Al Baqara 185:

يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.

Yanayofunguza.
1.Kuingiza kitu:-
Nako ni kuingiza kitu kutoka nje ya mwili mpaka ndani kwa kutumia njia zilizo wazi, na huingia katika hilo vinywaji, vyakula, dawa ya kunyunyiza puani n.k.

2. Kutoa kitu:-
Nako ni kusababisha kutoka vilivyo tumboni kama vile kujitapisha; atakae sababisha kujitoa matapishi kwa kuingiza kidole chake kwenye koo anahesabika amefunguwa; todauti na vinavyotoka tumboni vyenyewe bila ya hiari au kusababisha kwani hivi havipelekei kutengusha saumu.

3. Kuingiliana:-
Nako ni kufanya kitendo cha ndoa kwa kuingiliana tupu mbili, vilevile kukusudia kujitoa manii, na kunapewa hukumu hiyo kujitoa manii kwa kujichezea utupu.

4. Maasi:-
Na dalili ya hili ni hadithi ya Mtume wa Allah S.A.W
“Na hapana saumu isipokuwa kwa kuacha aliyo haramisha Allaah”.

Kuwa na nia: Hana saumu ambae hakunuia tangu usiku, na maana ya kunuia ni kuazimia moyoni; asiyeazimia kufunga kabla ya kuchomoza al-fajri basi hana saumu.

Kujua kuwa uwo katika saumu:-
Ikitokea aliyefunga amekula au amekunywa kwa kusahau, basi saumu yake haiharibiki; kwani kuna hadithi kuwa Mtume wa Allaah S.A.W amesema:

“Atakae kula au kunywa kwa kusahau basi akamilishe saumu yake; kwani Allaah ndie aliyemlisha na kumnywesha”

Kuchomoza Al Fajri yakweli:
Kwa dalili ya maneno ya Mwenyezi Mungu ktk surat Al Baqara aya 187.

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ.
Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajri katika weusi wa usiku.

Mpaka kuzama kwa jua Maghrib;
Kwa dalili ya maneno ya Mtume S.A.W 
“Unapo ingia usiku kwa huku na ukaondoka mchana kwa huku, aliyefunga kafungua”

Tunamuomba ALLAH azitakabalie saumu zetu.
Amin.

Faidika na Mawaidha


Ratiba ya mwezi wa Ramadhani
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top