Kiongozi wa LRA Joseph Kony.
Karibu wapiganaji 50 wanaoamika kutoka kundi la Lord's Resitance Army (LRA) la nchini Uganda, waliendesha uvamizi mishoni mwa wiki katika eneo lililo umbali wa kilomita 500 kaskazini mwa mkoa wa Kisangani nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.
Karibu watu 100 wanaaminika kutekwa nyara wakati wa uvamizi huo. Wale waliotekwa wanaripotiwa kulazimishwa kubeba mali ambayo wapiganaji hao walikuwa wamepora.
Wanafunzi ambao walikuwa wamesafiri kutoka vijiji vilivyo karibu kuja kufanya mtihani wa kitafa wa shule ya msingi, wakiwemo wafanyibiashara na wauguzi waliokuwa wakitoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa uti wa mgongo, ni kati ya wale waliotekwa nyara.
Usimamizi wa eneo la Bondo ambapo kisa hicho kilitokea, unasema kuwa wanajeshi wamewafuata wapiganaji hao kwenda msitu wa Adama yaliko maficho yao.
Kundi la LRA lilianzishwa nchini Uganda karibu miongo mitatu iliyopita, lakini likahamia nchi zingine majirani kutokana oparesheni iliyokuwa ikiendeshwa na jeshi la Uganda.