JICHO LA 3: MO BEJAIA 1-0 YANGA, ‘WAKIMATAIFA WANAOISHI KATIKA FIKRA ZA MCHANGANI’


Kuelekea mchezo wao wa kwanza wa CAF Confederations Cup 2016, mabingwa wa Tanzania walijitahidi kufanya kila jitihada kuhakika wanapata kambi bora yenye utulivu, na walitua Bejaia, Algeria wakitokea nchini Uturuki walikoweka kambi ya wiki moja.

Mashabiki wengi wa Yanga waliamini timu yao itapata ushindi kulingana na wapinzani wao MO Bejaia kutokuwa na uzoefu mkubwa katika michuano ya vilabu barani Afrika, hata mimi niliamini kikosi cha M-holland, Hans Van der Pluijm kingepata ushindi wake wa kwanza dhidi ya timu za Kiarabu ugenini.

Kikosi ambacho Hans alikianzisha tayari kilikuwa katika mawazo yangu siku moja kabla. Niliamini timu itashambulia kwa kuwategemea Oscar Joshua katika beki 3 na Mbuyu Twite katika beki namba 2.

Niliamini Deo Dida atalindwa vizuri na Kelvin Yondan na Vicent Bossou na safu hii ya ulinzi licha ya kuruhusu goli lililotokana na shambulizi la haraka lililokamika dakika ya 20′, kwa pamoja watano hawa walifanya kazi nzuri katika ulinzi.

Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima walijitahidi kuilinda timu na kudhibiti mpira ndani ya dakika 30′ za kwanza ambazo wenyeji walifanya mashambulizi mengi. Viungo hao wa kati waligeuka ‘mwiba’ kipindi cha pili, lakini bao la mlinzi Salhi Yassine liliwaongezea nidhamu zaidi ya kujilinda MO Bejaia hasa wakitambua TP Mazembe ilikuwa imeshinda 3-1 katika mchezo wa mapema wa kundi A.

Kiujumla timu ilizidiwa sana dakika 25 za kipindi cha kwanza lakini uwezo mdogo wa kimbinu wa Bejaia uliwafanya Yanga kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa goli 1-0, matokeo ambayo yalisimama hadi mwisho licha ya jitihada kubwa za Deus Kaseke, Amis Tambwe, Donald Ngoma na Saimon Msuva.

Timu ambayo ilifunga magoli manne dhidi ya Al Ahly na Esperanca imeshindwa kufanya hivyo katika mazingira ambayo si rahisi kuamini, ila ndiyo ‘mpira wa miguu.’

MAMBO MAKUBWA MAWILI YAMECHANGIA…

Yanga kupoteza mchezo wake wa kwanza usiku wa kuamkia leo. Baada ya jitihada zote kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanafanya maandalizi yao kwa uhakika, uhuru na usalama, uongozi ulipatia kuipeleka timu Uturuki lakini ni wao walioiangusha timu.

Kitendo cha kuingia madukani kununua jezi mpya za kutumia katika mechi dhidi ya Bejaia ni dalili za utendaji mbovu. Hapa napatwa na mshangao kiasi kwa maana CAF waliwakataza Yanga kutumia jezi zao zilizozoeleka zikiwa na nembo ya mdhamini wao ‘Bia ya Kilimanjaro’ kifuani.

CAF wanasema klabu hazitakiwi kuweka chata za wadhamini wao sehemu kubwa ya wazi katika jezi, kwa mujibu wa kanuni zao lakini ni ukiritimba tu wa kanuni mbovu katika michuano mingi ndani ya Afrika. Yaani, mdhamini ambaye amenisaidia kufika hapo nilipo, anakataliwa na kanuni tu wakati malengo makubwa ya wadhamini ni kujitangaza na kutangaza biashara yao.

Kama wangesema sababu za kiimani sawa, wangeeleweka ila hivi si haki kwa wadhamini. Nawalaumu Yanga kwa kushindwa kuhudhuria semina elekezi ambayo CAF waliifanya kwa vilabu vyote 8 vilivyofuzu kwa hatua hiyo ya makundi.

Kama TP Mazembe wanahudhuria katika semina, Yanga pia walipaswa kufanya hivyo. Kwanza kwa ugeni wao, pia wangejua mapema ni jezi za namna gani zinatakiwa kutumiwa na klabu.

Kwenda Uturuki, kujiita wa Kimataifa, mabadiliko ya ghafla ya jezi za kutumia na kushindwa kuhudhuria semina elekezi ya CAF ambayo walitumiwa barua ya mwaliko ni kielelezo tosha kuwa hawa nao ni, ‘Wakimataifa wanaoishi katika fikra za mchangani…’

Kitendo tu cha kuambiwa ubadilishe jezi katika ‘Ndondo’ ikitokea kufanana kwa jezi za timu zote, huwa panachimbika.

Kwa nini? Ni kwa sababu katika fikra zetu Waafrika tunaamini ni mkosi, na kubadilisha jezi inachukuliwa ‘siriasi’ kama sababu ya kushindwa mchezo hata kabla ya kuanza kwa mchezo. Mambo kama haya yanashusha morali ya wachezaji na wakati mwingine yanavuruga saikolojia ya mchezaji kwa kufikiria sababu ya kutokea kwa yote hayo.

Kitendo cha CAF kuwazuia wachezaji wao wapya kucheza game ya jana usiku ni kielelezo kingine kuwa uongozi unapaswa kuamka zaidi. Walikosaje kuzungumza na Simba SC kirafiki na kuwaomba barua ya kumruhusu Hassan Kessy?

Kwa namna alivyocheza Mbuyu-alilinda vizuri lakini hakuwa bora katika mashambulizi, Kessy angecheza vizuri zaidi ya Mnyarwanda huyu. Juma Mahadhi kuna wakati Yanga ilikuwa ikimuhitaji mchezaji kama yeye ili wapate goli lakini naye akapigwa stop.

Kuwakosa Mahadhi na Kessy dakika za mwisho naamini kulivuruga mbinu za mwalimu Hans lakini hataweza kusema. Umakini mdogo wa uongozi au pengine uzoefu wao mdogo kimataifa ndiyo sababu ya kuanguka kwa Yanga mbele ya MO Bejaia. Safari bado inaendelea ila tujifunze kutokana na makosa yetu wenyewe. ‘Bora Kuliko’ inakuja Dar es Salaam.

Ni wakati wa Jerry Murro kufanya kazi yake vizuri na si kuchekesha watu kila mara. Murro anapaswa kupita pita katika mitandao ya wapinzani wao, CAF atapata faida ya kuisaidia zaidi timu yake. Hans pekee na benchi lake la ufundi hawatoshi.
 
Like page yetu ya facebook upate habari kwa urahisi na haraka zaidi BOFYA HAPA

HABARI KUU LEO BOFYA HAPA

Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top