Huu ndio Msimamo wa Julius Mtatiro kufuatia hatua ya Prof Lipumba kutengua uamzi wake


NGOJA NIWAELEZE UKWELI!

Kama mzee wetu anao washauri, wamwambie kuwa "DALILI ZA MVUA NI MAWINGU". Na kwamba, NGOMA ivumapo sana hupasuka na tena ajulishwe kuwa VITANI hakuna michezo ya KUJIFICHA na KUONEKANA baadaye, jana niliwaambia kuwa najua CUF inao watu makini wanaojua nini haki ya PROFESA LIPUMBA na nini haki ya CUF kama chama.

Kwa wale ambao hawakuelewa ujumbe wangu wa jana nilikuwa namaanisha viongozi wa CUF watakuwa upande wa chama, hawatafuata matakwa ya mtu, na dalili zimeanza kuwa hivyo. Mwisho wa siku mshindi wa mchezo huu ni CHAMA na WANACHAMA wenye UTII na COMMITMENT kwa chama chao, na siyo MTU!


Ukweli ni kuwa CUF ni taasisi imara na haiwezi kuwa na MBAO za kugawana. Kutakuwa na machaguo mawili tu, aidha kuondoka na mtu au kubaki na chama, wale watakaobaki na chama watabaki na mbao zote, na wale watakaoondoka na mtu hawatandoka na hata kipande cha ubao. Siasa ni maisha halisi ya watu, vyama vikiruhusu zigeuke kuwa mchezo wa KOMBOLELA, zitakosa maana.

Profesa Lipumba ambaye kila mtu anamheshimu sana, apishe kwenye uongozi ili chama kijiandalie ZAMA mpya. Nawarejesha kwenye nukuu yangu ya mwaka jana wakati anajiuzulu, kwamba "Kamanda wa vita akiuawa katikati ya vita, siyo muda wa kuanza kulia na kuomboleza, siyo muda wa kulaumiana, anatafutwa askari mwingine na kutwaa bunduki yake, mapambano yanaendelea mbele".

Namshauri Prof. Lipumba, kwa namna yoyote ile, asikubali kutumikia matakwa ya kundi lolote lile, iwe ndani ya chama au nje ya chama. Asikubali kuwa sehemu ya kuanzisha mgogoro na vurumai kubwa ndani ya chama, asikubali kuwa chanzo cha kuleta sintofahamu kama hii, namtambua Mwenyekiti wangu kama mtu makini na mtu mwenye upeo wa kipekee, hebu na autumie kuonesha busara na ukomavu.

Binafsi nisingelipenda kuona mgogoro mwingine mkubwa CUF, ambao matokeo yake sote tunayajua, kwamba chama ndicho kitashinda na kitabaki salama salmini, na kwamba watu wachache ndiyo wataumia na kufedheheka, akiwemo mtu anayeheshimiwa sana na aliyewahi kushiriki kukijenga chama hiki kwa nguvu zake na akili zake zote.

Mtatiro J
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top