Ureno na Austria wanakutana leo katika hekaheka za kuwania ubingwa wa michuano ya Euro 2016, ukiwa ni mchezo wa pili wa kundi F utakaofanyika katika dimba la Parc des Princes jijini Paris majira ya
saa nne usiku.
Huu ni mchezo unaotarajiwa kuwa wa kuvutia kwa sababu tofauti tofauti. Kabla ya kuanza kwa mashindano haya, watu wengi walitarajia timu hizi mbili zingemaliza kileleni mwa kundi kutokana na ubora wao. Lakini kwa nama msimamo ulivyo kwa sasa, wote wanaweza kujikuta nje ya kinyang’anyiro endapo inatokea mmoja kati yao anapoteza mchezo wa leo.
Austria walipoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 2-0 na Hungary, mchezo ambao timu zote zilicheza kwa kufunguka na kushuhudia wakifanya ‘attempts’ 14 katika mchezo wote. Safu ya ulinzi ya Austria ilionekana kuwa na udhaifu baadhi ya sehemu na pengine kama hawatajirekesbisha Ureno wanaweza kutumia mwanya huu kuwaadhibu.
Bila shaka Ureno watakuwa na dhumuni la kumaliza mchezo wa leo kwa ushindi kutokana na kushindwa kufanya hivyo katika mchezo wa awali dhidi ya Iceland ulioisha kwa sare ya 1-1.
Ureno walifanya mashambulizi mengi ikiwa ni pamoja na kupiga mashuti 26 huku nane tu kati ya hayo yakilenga lango la wapinzani wao na Ronaldo pekee akipiga mashuti 10 na moja tu ndio lililenga langoni huku sita yakizuiwa.
Hata hivyo bado Ronaldo alikuwa na mchezo mzuri baada ya asilimia 90 ya pasi zake zote kufanikiwa kuwafikia wahusika na kuleta nyingi kati ya hizo zilileta hatari kubwa langoni mwa Iceland.
Ureno
Kocha Fernando Santos yuko tayari kukifanyia mabadiliko kikosi chake baada ya hapo awali kukiri kuwa anapaswa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji.
Renato Sanches anaweza kuanzia benchi huku Ronaldo akitaka kuvunja rekodi ya Figo ya kucheza michezo mingi (127).
“Austria ni timu imara, wana uwezo mkubwa wa kushambulia kutokana na kuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa. Wana tofauti kubwa na Iceland,” anasema kocha wa Ureno Fernando Santos
“David Alaba, Marko Arnautović, Marc Janko, Martin Harnik … wote ni wachezaji wa kiwango cha juu bila kusahau Zlatko Junuzović. Austria ni timu aina ya timu ambayo wachezaji wake wanautaka mpira muda wote.”
“Hatupaswi kuchunga mchezaji mmoja mmoja bali timu nzima kwa ujumla. Tulicheza vema dhidi ya Iceland. Tunapaswa kufanya marekebisho madogo ili tuweze kupata matokeo kwenye mchezo wa leo.”
Austria
Kocha wa Austria Marcel Koller anasema: “Tunapaswa kucheza tofauti na namna tulivyocheza kwenye mchezo wetu dhidi ya Hungary.
Anaongeza: “Tumefanya upembuzi na kujifunza kutokana na makosa tuliyofanya, tunapaswa kuwa makini na nafasi zote tutakazopata lakini vile vile kuwa na umakini katika safu yetu ya ulinzi.”
“Tunafahamu kuwa Ureno sio tu Cristiano Ronaldo. Wana wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kuamua matokeo ya mchezo licha ya kwamba Ronaldo ni kinara wao.
Rekodi zao katika mechi walizokutana.
Ureno wameshinda michezo 2 tu kati ya 10 ya mwisho waliyokutana na Austria (Droo tano, wamepoteza michezo mitatu).
Austria waliwafunga Ureno 9-1 mjini Vienna katika hatua za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 1954.
Ushindi wa mwisho wa Austria dhidi ya Ureno ulikuwa ni mwaka 1979, walipowafunga 2-1 wakati wa kufuzu michuano ya Ulaya jijini Lisbon. Mara ya ,mwisho kukutana ilkuwa ni mwaka 1995 na mchezo kuisha kwa sare ya 1-1.
Fernando Santos akiwa kocha wa Ugiriki aliwafunga Austria 2-1 kwenye michezo ya kirafiki uliochezwa November 2010 na 2-0 August 2013.
Austria wameruhusu goli moja dhidi ya Ureno katika kila mchezo kati ya michezo yao mitano ya mwisho waliyocheza.
Ureno
Ureno wamefanikiwa kuvuka hatua ya makundi mara zote sita zilivyopita ambapo walishiriki michunao hii.
Hawajashinda mechi za ufunguzi katika michuano mikubwa tangu mwaka 2008 (droo 2, wamepoteza mara mbili)
Wameshinda mara moja tu katika michezo yao mitano iliyopita (droo tatu, wamefungwa mchezo mmoja)
Goli la Nani katika mchezo dhidi ya Iceland, lilikuwa ni la 600 tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo.
Cristiano Ronaldo atakuwa mchezaji wa Ureno aliyecheza michezo mingi zaidi katika historia ya timu hiyo kama akicheza mchezo wa leo. Kwa sasa analingana na Luis Figo kwa kucheza michezo 127.
Austria
Hawajawahi kupata ‘clean sheets’ kwenye michuano hii, wakiruhusu walau goli moja katika kila mchezo kati ya michezo minne.
Austria wameheza michezo 13 bila ya ‘clean sheet’ katika michuano mikubwa. Mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni mwaka 1982 kwenye Kombe la Dunia dhidi ya Algeria.
Kati ya mashuti 28 waliyopiga katika michuano hii ya Ulaya, hakuna hata moja lililoingia golini.
Austria wamepoteza michezo mitatu kati ya minne ya mwisho (ikiwemo ya kirafiki). Ushindi wao wa mwisho ulikuwa dhidi ya Malta.
HABARI KUU LEO BOFYA HAPA