Chadema Wajifungia Kujadili hatua za kuchukua Dhidi ya Jeshi la Polisi Lililopiga Marufuku Maandamano na Mikutano

Viongozi wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Vincent Mashinji jana walijifungia kutwa nzima kujadili hatua za kuchukua dhidi ya kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mikutano ya chama hicho ya kisiasa.


Tangu asubuhi jana, viongozi hao walikuwa na kikao katika ukumbi wa Mandela, hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza na wakati wa mapumziko mafupi saa kumi jioni, Mbowe alisema chama hicho kitatoa kauli rasmi leo baada ya kikao kingine kilichotarajiwa kufanyika jana usiku.


“Tutatoa kauli rasmi kesho (leo), baada ya vikao. Ninachoweza kuthibitisha ni kwamba tunaendelea kushauriana njia sahihi ya kuchukua,” alisema Mbowe.


Juni 7, mwaka huu polisi ilitangaza kupiga marufuku kwa muda usiojulikana maandamano na mikutano yote ya kisiasa kwa kile kilichodaiwa ni taarifa za kiintelijensia za kuwapo tishio la kiusalama na kuwa wanakwenda kushawishi wananchi kuipinga Serikali.


Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema miongoni mwa masuala ya msingi yaliyokuwa yakijadiliwa jana ni pamoja namna bora na sahihi ya kuendelea kufanya shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara bila vikwazo.


“Katika hili, tutatumia mbinu zote kuanzia zile za kisiasa, kisheria na kijamii,” alisema Mwalimu.


Ingawa hakuna kiongozi wa Chadema aliyekuwa tayari kukanusha wala kuthibitisha kilichosababisha vikao vyao vya jana kuchukua muda mrefu na mvutano miongoni mwa wajumbe kuhusu hatua za kuchukua.


Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina , mmoja wa wajumbe alisema baadhi ya wajumbe walitaka chama hicho kuendelea na ratiba yake ya mikutano ya hadhara bila kujali zuio la polisi walilosema halina misingi ya kisheria, isipokuwa jeshi hilo linatumika kisiasa kuhujumu vyama vya upinzani kwa maslahi ya chama tawala cha CCM.


“Baadhi yetu, nikiwamo mimi tulitaka chama kutumia mkondo wa kisheria kupinga zuio hilo badala ya kuendelea kutunishiana misuli na polisi,” alisema mtoa taarifa wetu.


Baadhi ya mawakili wa Chadema, akiwamo Paul Kipeja, John Mallya, jana walionekana katika viunga vya hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza katika kilichoelezwa na vyanzo vyetu kuwa ni maandalizi ya chama hicho kufungua shauri mahakamani dhidi ya Jeshi la Polisi.
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top