ALVES ANAONDOKA BARCA NA KUACHA ALAMA 16 ZA KUKUMBUKWA


Dani Alves ni moja ya wachezaji waliocheza Bracelona kwa mafanikio makubwa sana. Ameitumikia kwa uaminifu klabu hiyo kwa takriban misimu nane. Alves anaondoka rasmi Barcelona na kuelekea Juventus ya nchini Italy. Baada ya msimu huu kumalizika, aliandika ujumbe mzito sana kuwashukuru mashabiki, wachezaji pamoja na viogozi wa Barcelona. Katika kipindi chote alichodumu klabuni hapo amefanya mambo makubwa sana, lakini haya ni baadhi kati ya hayo yote.
Alves alijiunga na Barcelona katika usajili wa majira ya joto mwaka 2008 baada ya kuitumikia Sevilla kwa miaka sita kipindi hicho akiwa na miaka 25. Wakati akijiunga na Barcelona aliyekuwa rais wa Barcelona Joan Laporta alimtunuku kama ‘beki bora wa kulia duniani’ akithibitisha ubora wake kutokana na ada ya Euro milioni 35 aliyonunuliwa. Ada hiyo ya uhamisho ilimfanya Alves kuwa mchezaji wa pili kununuliwa kwa kitita kikubwa zaidi katika historia ya timu hiyo kwa wakati huo.
Katika mchezo wake wa kwanza alianza na kikosi chenye wachezaji hawa: Golini alikuwa Victor Valdez, kulia Alves mwenyewe, kushoto Erick Abidal, nne na tano kulikuwa na Carlos Puyol na Marquez, nafasi ya kiungo kuliwa na Xavi Hernandez, Yaya Toure na Andres Iniesta, safu ya ushambuliaji iliundwa na Lionel Messi, Thierry Henry na Samuel Eto’o.
Goli lake la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya Almeria Oktoba. Katika mchezo huo, Samuel Eto’o alipiga hat-trick huku goli lingine likifungwa na Thierry Henry.
Alves alishiriki kikamilifu kuweka historia msimu wa 2008/09, akiwa moja ya wachezaji waliofanikisha kuipa Barcelona makombe matatu kwa mpigo kwa msimu (treble). Akiwa chini ya Pep Guardiola, Alves alicheza michezo ya ligi 34, 12 ya UEFA Champions League na nane ya Copa del Rey.
Akiwa na Barca kwa msimu wake wa pili, Alves alifanikiwa kufikisha michezo 100 ambapo ilikuwa ni Mei 4, 2010. Katika mchezo huo dhidi ya Tenerife Barca walishinda magoli 4-1, ambapo Alves alitoa pasi mbili za mabao (assists), moja kwa Bojan na nyingine kwa Lionel Messi.
Januari 25 katika dimba la Cam Nou, kwa mara ya kwanza Alves alifanikiwa kuwafunga Real Madrid baada ya kuachia shuti kali kutoka nje ya penati boksi na kutinga wavuni. Hiyo ilikuwa ni katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Mfalme (Copa del Rey) ambapo Barca walifanikiwa kusonga mbele.
April 3, 2012, katika mchezo wa nusu fainali ya UEFA Champions League dhidi ya AC Milan, Alves alifanikiwa kutimiza michezo 200 akiwa na Barca huku akiweka kibindoni magoli 15 mpaka siku hiyo. Katika mchezo huo Barca walishinda mabo 3-1, mchezo uliochezwa katika dimba la Camp Nou.
Katika msimu wa 2013/14, Alves aliamua kubadilisha namba ya jezi yake na kuvaa namba 22 akii-dedicate kwa Erick Abidal ambaye alikuwa akiondoka kutokana na matatizo ya afya yaliyokuwa yakimsumbua. Abidal alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya ini.
Msimu huo huo wa 2013/14, Alves alikuwa nyota wa mchezo wa 16 bora kati ya Barcelona na Manchester City. Akifunga katika mechi zote mbili. Mchezo wa kwanza walishinda magoli 2-1, wa pili walishinda magoli 2-1.
April 20 mwaka 2014, katika mchezo dhidi ya Athletic Club Bilbao kwenye dimba la Camp Nou, Alves alimzidi Phillip Cocu na kuwa wa pili katika orodha ya wachezaji wa kigeni waliocheza mechi nyingi zaidi katika historia Barcelona kwa kucheza michezo 293. Kuondoka maana yake ni kwamba Lionel Messi ataendelea kushikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kwa kucheza mechi 531. Alves ameondoka Barca akiwa amecheza michezo 391.
Msimu wa 2014/15, Alves alisherehekea kutimiza michezo 300 akiwa na Barcelona katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya APOEL.
Msimu wa 2015/16, Alves alirudia tukio la kubadilisha namba ya jezi kwa mara nyingine tena baada ya kuamua kuachana na jezi namba 22 iliyokuwa ya Abidal na kuvaa jezi namba sita maalum kwa ajili ya kumuenzi Xavi ambaye ni Legend wa klabu hiyo aliyekuwa akiondoka.
Kuondoka kwa Alves inawezekana ni habari mbaya sana kwa Barcelona, lakini mbaya zaidi kwa Messi ambaye ndiyo amepata pasi nyingi za magoli (assist) kutoka kwa Dani Alves kwa kipindi chote cha miaka nane aliyohudumu klabuni hapo.
Goli lake la mwisho alifunga katika msimu wa 2015-16, katika mchezo wa Copa del Rey dhidi ya Villanovense. Msimu huo pia alichangia kwa kiasi kikubwa Barcelona kuchukua treble.
Katika kipindi kisichopungua wiki mbili kabla ya kutangaza kuondoka kwake, Alves alicheza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Sevilla kwenye kombe la Copa del Rey, ambapo Barca walishinda na kuchukua kombe hilo. Ikumbukwe mchezo huo ulikuwa na maana kubwa sana kwake kutokana na kucheza na Sevilla, timu ambayo ilimtambulisha katika ulimwengu wa soka la Ulaya.
Sasa ni rasmi anaondoka Barcelona akiwa ameacha historia kubwa. Kwa muda wake wote klabuni hapo, ameshinda kila kombe ngazi ya klabu. La Liga mara sita. Champions League matatu, Copa del Rey matatu, European Super Cup matatu, Spanish Super Cup manne na matatu ya Club World Cup.
Credit:Dauda
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top