Najua nazungumza na mabilionea wakubwa, kama si mabilionea wa sasa, basi ni
mabilionea wa baadaye. Wewe ni bilionea, nakutamkia hili na unatakiwa kuamini pasipo kujali kwamba kwenye akaunti una shilingi elfu moja au chini ya hapo, unachotakiwa kuamini kwamba wewe ni bilionea.
mabilionea wa baadaye. Wewe ni bilionea, nakutamkia hili na unatakiwa kuamini pasipo kujali kwamba kwenye akaunti una shilingi elfu moja au chini ya hapo, unachotakiwa kuamini kwamba wewe ni bilionea.
Inawezekana umeanzisha biashara yako, kitu cha ajabu kabisa, fedha hazikai, kila ukipata leo, kesho hazipo, ili kuendesha biashara yako inakupasa kukopa sehemu, ni kweli ulipata faida, ila kwa nini ukope? Kopa wakati ukitafuta mtaji, ila kama umeshafanya biashara na faida ukapata, kwa nini ukope? Kwa nini usitumie faida uliyoipata kukuinua hapo ulipo?
Wengi wanakutana na hali hiyo, si wewe tu, hata mimi nilishawahi kukutana nayo, na si sisi tu, amini hata mabilionea wakubwa walishawahi kukutana na hali hiyo. Hivi unajua ni mabilionea wangapi waliwahi kufilisika? Unamjua Muitaliano Enzo Ferrari? Alipata fedha, akafilisika, akagundua alipofanya makosa, akatafuta tena, akazipata.
Wewe kama binadamu wengine, unaweza kupata fedha na kufilisika, hapa siwazungumzii wakina Bakhresa, Mengi na wengineo, nakuzungumzia wewe mwenye biashara ndogo, nataka biashara yako ikue, utoke hapo ulipo na usogee mbele zaidi, ufanikiwe na siku moja uitwe bilionea Omari, Selemani, John, Hamisi, Sara, Anna, Peter au jina lolote ulilokuwa nalo.
Hizi ni baadhi ya njia ambazo zinaweza kukusaidia kufikia ubilionea japokuwa una biashara ndogo au kipato kidogo.
1. WEKA MALENGO: Kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya kama mfanyabiashara ni kuweka malengo. Hebu chukua karatasi, andika malengo yako na kuyafanyia kazi. Kumbuka wewe ni bilionea, usiweke malengo ambayo unadhani kwamba pia ua utayafikia, ukiyaandika hayo, jua hautotoa nguvu kubwa kupambana ili uyafikie malengo hayo. Kama una mtaji mdogo, weka malengo makubwa ya kufanikiwa, unapoweka malengo makubwa zaidi ya ulichonacho kitakufanya ujitoe zaidi, uongeze juhudi ili kufikia kile unachokiwazia.
Mfano wewe ni mfanyabiashara mdogo, ukaweka lengo kwamba mpaka mwaka kesho lazima uanzishe biashara ya kuuza mahindi mitaani. Sawa, si vibaya lakini ulitakiwa kuweka malengo ya biashara kubwa zaidi. Kwa fedha hizohizo ulizokuwa nazo, unaweza kuanzisha biashara ya mahindi, ukijiwekea hivyo, jua kwamba unayachelewesha mafanikio yako. Ninataka ujitume kwa nguvu zote, ukiweka yale malengo makubwa, utajiona huwezi kufika lakini ndiyo yatakayokufanya kupambana zaidi, hutolala, utapambana usiku na mchana ila ukiweka lengo dogo, utasema subiri upumzike kwani lengo hilo litakuja hata kama hutojitoa, hivyo ili ufanikiwe, jiwekee lengo kubwa na hakika utapiga hatua.
Mfano mzuri mimi. Sikuwa na fedha kipindi cha nyuma, ishu ya kuanzisha magazeti ilihitaji msingi mkubwa sana, ila sikutaka kukwepa lengo langu la kufanya hivyo. Ningeweza kusema niuze machungwa mitaani, kweli ningeuza, lakini kwa nini niweke lengo dogo? Je ningejitoa zaidi? Ili nijitoe, ili nifanye kazi usiku na mchana ilikuwa ni lazima niweke lengo kubwa, nikaweka, nikajitoa na kufanikiwa. Kama Shigongo, yule mtoto masikini ameweza, vipi kuhusu wewe?
2. USIOGOPE KUFELI: Ndiyo! Kuna watu waoga sana, wanaogopa kufanya biashara fulani kubwa kwa kuwa wanaogopa kuanguka. Rafiki yangu, kuanguka ni sehemu moja ya maisha, ili usonge mbele ni lazima uanguke. Huwezi kujua kuendesha baiskeli kama hujaanguka, ni lazima uanguke ili ujue, iko hivyo.
Mtoto anapoanza kutembea, kuna kipindi anaanguka, mbona yeye hakati tamaa na kusema kwamba kuanzia leo hatembei tena kisa ameanguka? Akianguka, hunyanyuka na kutembea tena, akianguka anajaribu tena.
Wewe kama mfanyabiashara mdogo au mkubwa, jifanye mtoto, usiogope kufeli, ili usonge mbele, ni lazima ufeli, huwezi kuwa mshindi siku zote, kuna kipindi unashindwa, ukishindwa, unakaa chini na kuwaza umeshindwa wapi, unajipanga na kurudi tena kwenye gemu.
Kama ningekuwa naogopa kufeli, nakwambia ukweli kwamba nisingekuwa hapa, labda leo ningekuwa mtaani tu nafanya biashara ndogondogo, kuogopa kufeli kungenifanya niwe kulekule nilipokuwa nyuma. Ili ujifunze, ili upige hatua ni lazima ufeli, ukifeli, unajifunza na kusonga mbele.
3. WEKA UMAKINI NA FEDHA ZAKO: Siku zote nimekuwa nikiwaambia watu, si vizuri kutumia kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya unachoingiza. Mwingine ana biashara inaingiza elfu ishirini kwa siku, ila anataka kufanya matumizi yasiyokuwa na faida kwa kutumia elfu thelathini. Ndugu yangu! Huwezi kuishi kwa maisha haya halafu ukaja kufanikiwa. Unatakiwa kuwa makini na fedha zako.
Mwingine anasema, nimepata faida nyingi, acha nikale bata! Ndugu zangu, bata haziishi, kila siku zinaongezeka, baa hazifungwi, umezikuta na utaziacha, kumbi za starehe kila siku zinafunguliwa mpya.
Ithamini pesa yako, hata kama ni shilingi hamsini, ithamini. Unapokuwa na elfu moja, inayokamilisha hela hiyo ni shilingi hamsini, kama ukiwa na 950, huwezi kupata 1000 kama huna hamsini, kwa hiyo kwenye maisha yako ya kibiashara, hata shilingi 50 ni muhimu mno kwako.
Usiipuuzie fedha yoyote ile, panga matumizi yako ya kawaida, si muhimu sana kunywa soda kama huna sababu ya kufanya hivyo! Hakuna umuhimu wa kula chipsi kuku kama hakuna umuhimu wa kufanya hivyo! Kwani usipokula chipsi kuku utakufa? Kama una kiasi kidogo cha fedha basi hata matumizi ya fedha yako hakikisha yanakuwa madogo na si makubwa zaidi ya kile ulichokipata.
4. JENGA URAFIKI NA WENYE FEDHA: Hapa simaanishi kwamba wasiokuwa na fedha inabidi watengwe, hapana! Ila unatakiwa kuwa makini, ni vizuri kutengeneza marafiki wapya lakini inabidi uwe makini. Kabla ya kuwa nilivyo niliwahi kuwasikia watu wakisema unapoanza kufanikiwa unabadilika, nilipinga lakini nikaja kuona inawezekana.
Unapokuwa umefika hatua fulani, automatic unaanza kutafuta watu ambao wanaweza kukuvusha kutoka hapo ulipo, watu wenye uwezo wa kukufanya kufanikiwa zaidi. Kumbuka shuleni kwenu, ni wanafunzi wangapi waliokuwa na akili walikuwa marafiki wao kwa wao? Kwani hawakuwa marafiki zako pia, walikuwa marafiki zako ila wenyewe wakawa beneti, ipo hivyo.
Unapopata fedha, unapofanikiwa, jaribu kutengeneza ukaribu na watu waliofanikiwa, usiwaache wale wengine, kuwa nao ila usiwe nao beneti kupindukia, kama unaona mtu haeleweki, hana hamasa ya kukufanya kufanikiwa, kwa nini uwe naye beneti? Muache awe rafiki wa kupiga naye stori dakika kumi na kuondoka.
Unapokuwa siriazi kutafuta fedha, huna budi kuwatafuta waliofanikiwa, wakufundishe kwa nini wapo hapo, walipitia nyanja zipi mpaka kufanikiwa hivyo? Ni lazima ujifunze kupitia wao na hakika utafanikiwa.
5. USICHANGANYE BIASHARA NA URAFIKI/NDUGU: Ndiyo! Wengi tunafeli hapa. Tunapopata nafasi ya kufanya biashara, wengi tunakosa kufanikiwa kwa sababu tu tumechanganya urafiki katika biashara. Biashara ndogo lakini bado unataka kukopesha, tena kwa watu ambao huna uhakika kama watakulipa.
Unapoanzisha biashara, wengi watakuja kukopa na si kununua, hebu jiulize, wakati hujaanzisha hiyo biashara, mbona hawakuwa wakienda kukopa sehemu nyingine? Jua sisi binadamu tuna makusudi, tunapomuona mtu ameanzisha biashara, mara nyingi tunataka kumuangusha chini ili tumcheke, tumdhihaki kwamba kiko wapi sasa! Unatakiwa kuwa makini sana, huu si muda wa kupeleka urafiki na undugu katika biashara. Unapoanzisha biashara na ikatokea umemuajiri ndugu yako, mwambie wazi kwamba upo kama mfanyabiashara na si kama ndugu, anapofanya makosa, mchukulie hatua kama unavyomchukulia mtu baki, ukimuacha kwa kuogopa lawama, huyohuyo baadaye atakuja kukucheka.
Unapoona una hamu ya kula chipsi, na wewe unaifanya biashara hiyo ya chipsi, nunua chipsi zako, si kwamba ni zako basi na wewe ule bure. Najua ni ngumu kwa watu wengine lakini inabidi ufanye hivyo ili kuifanya biashara yako isimame.
Leo unapouza chipsi na kula bure, amini kwamba kesho utataka uongeze na chipsi yai, keshokutwa chipsi samaki, sasa ukifanya hivyo, hutofanikiwa kwa hiyo ni lazima hata wewe mwenyewe ujidai.
Sina mengi, ila tukutane muda mwingine kwa makala nyingine ya ujasiriamali. Kumbuka, wewe ni bilionea, fanya mambo kama bilionea.
Credit:E. J SHIGONGO
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)