JE, WEUSI WALIMUUNGA MKONO OBAMA KWA SABABU ZA KIHISTORIA?


Msomaji, kama umekuwa mfuatiliaji wa kuyasoma makala yangu haya ya kwanza, napenda kukumbusha tu kwamba makala haya mpaka sasa yamekufafanulia kuwa demokrasia ni utamaduni na mbinu (a technique) kwa 
madhumuni ya kudhibiti utawala/uongozi wa mabavu au ki-imla au hali ya utawala/uongozi wa bora liende; na sababu za kujifunza demokrasia kutoka Amerika.

Zaidi, yamekufafanulia kuwa wengine waliyafikiria ya Seneta Barack Obama kuwa Rais Mweusi wa kwanza hapa Amerika kwamba yalitabiriwa; sifa za Seneta Baraka Obama zilizofanikisha kampeini na kumletea ushindi; na jinsi ubaguzi wa rangi ulivyoingilia mchakato wa kampeini.

Ninaendelea na huo ubaguzi wa rangi katika makala ya leo, ikiwa ni pamoja na kuonyesha endapo kizazi kipya cha wa-Amerika kimeachana na ubaguzi wa rangi; ubaguzi miongoni mwa Weusi; na tamati fupi.

Tumeona jinsi ambavyo Weusi wazito, hasa wa New York, walivyompigia debe Seneta Hillary Clinton. Lakini Seneta Barack Obama hakukata tamaa. Aliinuka na kusimama kidete kutetea kwa nini alikigombea u-Rais katika hotuba aliyoitoa mjini Philadelphia, Pennsylvania, kwa wa-Amerika wote. Alielezea kwa ufasaha hali ya ubaguzi wa rangi nchini Amerika. Wengi waliipima hotuba hiyo na kuipa nafasi ya pili walipoilinganisha na ya hayati Dk. Martin Luther King, Jr.: I Have a Dream!

Baadhi ya wa-Ulaya wengi walimwona Barack Obama kuwa ni Mweusi kutokana na kuwa na damu ya ki-Afrika.

Lakini kuna wachambuzi wengine wa mambo ya uhusiano wa ubaguzi wa rangi ambao wanaamini kuwa ubaguzi uliojitokeza kati ya wa-Amerika wenye asili ya Ulaya, kwa upande mmoja, na wale wa asili ya Afrika, kwa upande wa pili, ulikuwa ni wa kusutana tu. Haukuchimbua masuala yenye uzito mkubwa yanayogusa maslahi ya wa-Amerika wenye asili ya Afrika na baadhi ya mataifa mengine yasiyo ya asili ya Ulaya.

Kizazi kipya na ubaguzi wa rangi!

Kulingana na takwimu aminika, wapigakura wengi waliomuunga mkono Seneta Hillary Clinton walikuwa ni wa-Ulaya wenye zaidi ya miaka 50 hivi; waliamini kuwa uwezekano wa Seneta Barack Obama kuchaguliwa ulikuwa nadra. Kundi la Seneta Hillary Clinton likuwa ni la kizazi kizee – kundi la walio na umri zaidi ya miaka 40!(P.T)


Seneta Obama aliielewa Amerika ya leo na inakoelekea. Si Amerika ya vyama vya wafanyakazi wa viwandani (industrial-age). Si wenye kufuata wosia kutoka kwa viongozi wa dini makanisani, misikitini na mahekaluni. Si wenye kuwasikiliza wa-Bunge (Congress). Hao ndio waliomwunga mkono Seneta Hillary Clinton.

Kundi hili lilipikuliwa na kundi la Seneta Barack Obama, kutokana na mbinu mpya za kuhamasisha wapiga kura vijana wengi chini ya miaka 40. Amerika ya leo ni ya tabaka la wafanyakazi maofisini (service-industry unions) wenye umri chini ya miaka 40. Tabaka hili linazidi kuongezeka na kupanuka.

Seneta Barack Obama alifaulu sana kulitekenya tabaka hili na kulishawishi na kuamsha mori miongoni mwa mamilioni ya watu wenye kuwasiliana kwa njia za viselula na “sms”. Hao ndio waliomwunga mkono.

Tabaka hili lilijitokeza kusambaza ujumbe na kupiga kura, ikiwa ni pamoja na kuchangia kuanzia dola tano tano na zaidi kila wiki ili kutunisha mfuko wa kampeini bila kutegemea mapesa ya takrima na/au ya vigogo! Utaratibu wa kuandikisha na kuhamasiha vijana nao ulipamba sana kupitia njia ya uso kwa uso, kupiga hodi milangoni, viselula, simu za kawaida, barua pepe na “sms”.

Lakini wa kumsifia ni Dk. Howard Dean (aliyepigania Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2004 kwa tikiti ya Democrat Party na kushindwa katika mchakato wa mwanzoni (primaries) na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democrat wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2008) kwa kugundua mbinu ya mawasiliano ya teknohama ya ki-mtandao, hasa miongoni mwa vijana!

Ubaguzi miongoni mwa Weusi

Mwanzoni baadhi ya “vigogo” wa-Amerika Weusi hawakumuunga mkono Seneta Barack Obama alipotangaza kuwania nafasi ya u-Rais! Kulikuwepo pia Weusi wengine ambao waliomwonea wivu Seneta Barack Obama kuwania wadhifa wa u-Rais. Kwa mfano, Rev. Jesse Louis Jackson, Sr. (RainbowPUSH Coalition). Mtamkumbuka Rev. Jesse Louis Jackson, Sr. ambaye alikuja kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Sullivan, Arusha. Nadhani Rev. Jesse Jackson, Sr. amekuwa akihudhuria mikutano ya Sullivan tangu ilipoanzishwa.

Mkutanoni hapo Arusha Rev. Jesse Louis Jackson, Sr. alijikweza akiahidi kuwa alikuwa na vijana wengi sana Weusi ambao Tanzania ingeweza kuwatumia kama walimu nchini! Wengine tulishangaa sana tuliposikia kauli hiyo! Kwani tunajua kuwa mashule ya msingi na sekondari wasomapo watoto Weusi hapa Amerika yanaathirika kutokana na uhaba wa walimu kiasi cha Amerika kuwatafuta walimu nchi za nje (u-Jerumani, sehemu za u-Soviet ya zamani na u-Filipino)!

Mwanzoni, Rev. Jesse Louis Jackson, Sr. alimshutumu Seneta Barack Obama kwa kuwakosoa Weusi na kuwataka wanaume kutakasa nyumba na familia zao kwa kuchukua majukumu kamambe ya kuikomboa familia; kupambana na kuvunjika kwa ndoa kunakoathiri malezi na masilahi ya watoto; na kujazana kwa vijana Weusi katika majela kutokana na kuvunja sheria za nchi – kuna vijana wengi majelani (mbali ya idadi ya wale wenye vifungo vya nje) kuliko waliomo vyuo vikuu!

Kumekuwepo na kutoelewana miongoni mwa Weusi kuhusu ni nani “msemaji” wa umma wa Weusi. Kwa mfano, wakati wa mapumziko mafupi, kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari, Rev. Jesse Louis Jackson, Sr., bila kujua kwamba kinasa sauti kilikuwa kimetegwa live, alitamka maneno ya ajabu na soni kuwa wakati mwingine huwa anafikiria kumkata korodani au kumhasi Obama – kwa maneno mengine kumumaliza kabisa mbele ya Weusi wenzake!

Kauli hiyo ya Seneta Obama ilikuwa sawa na kauli ya Mweusi mwingine, msanii, mchekeshaji na mcheza sinema na televisheni Dr. Bill Cosby, ambaye alishutumiwa pia na baadhi ya Weusi wenzake kwa kile walichokiona na walichokitaja kuwa ni kudhalilisha utu na heshima ya mtu Mweusi hapa Amerika.

Kauli za akina Seneta Obama na Dr. Cosby dhidi ya akina baba Weusi wanaotelekeza familia zao ndicho kilikuwa kitovu cha “Maandamano ya Mamilioni” yaliyokitayarishwa na wakina Louis Farrakhan (The Nation of Islam) na huyo Reverend Jesse Louis Jackson, Sr. (RainbowPUSH Coalition).

Kwa nini Rev. Jesse Jackson alipinga kauli hiyo ya Seneta Barack Obama? Reverend Jesse Louis Jackson, Sr. alimwona Seneta Obama kama si Mweusi kamili, si mwenzao; ni mgeni mlowezi asiye na kauli ya kuwaasa, mithili ya wa-Chagga kumwita mtu wa namna hiyo, chasaka au kyasaka (m-Chagga yeyote utanisamehe endapo nimevuruga jinsi neno hilo linavyoandikwa).

Adhabu aliyofikiria Reverend Jesse Louis Jackson, Sr. ilikuwa ni ya kumhasi korodani zake zilizompa ujasiri wa kuthubutu (the audacity) kuzungumza kwa niaba ya Weusi! Wachambuzi wengine wanasema kuwa Rev. Jesse Louis Jackson, Sr. alijihami hivyo kutokana na wivu. Rev. Jesse Jackson aliwahi na kuangushwa kugombea u-Rais; amekuwa kiongozi ambaye amepitwa na wakati.

Lakini wakati wa mkutano wa Rais-Mteule Barack Obama wa kushukuru ushindi wake, Rev. Jesse Jackson, Sr. alionekana kuguswa sana kiasi cha kutiririka machozi mengi ya furaha au kujutia kwa nini siku hiyo haikuwa yake. Pengine, yote mawili.

Kwa kifupi, kuna ubaguzi wa ki-historia wa aina yake kati ya na miongoni mwa Weusi watokanao na utumwa. Kuna wale waliokitumikishwa mashambani. Hawa hawaoni soni kujitambulisha na Afrika. Kuna wale wanaotokana na walokifanya kazi ya u-pagazi majumbani, ambao wengi wa kike walizaliana na wa-Ulaya.

Hawa walokifanya kazi ya u-pagazi majumbani wanaona soni kujitambulisha na Afrika, eti, kwa kufanya hivyo ni kusahau sehemu yao ya u-Ulaya! Pia kuna Weusi wengine ambao wametoka Visiwa vya Karibe (Caribbean) na Amerika ya Kati na Kusini. Na pia tusisahau Weusi wa hivi karibuni kutoka Afrika!

Fikra kuwa Mweusi mwenye asili ya utumwa (asiye wa kutokana na u-pagazi) ndiye anaweza kuwa kiongozi wa Weusi kabla ya kumfikiria kiongozi wa namna hiyo wa kutokana na wa u-pagazi au wa kutoka Visiwa vya Karibe (Caribbean), Amerika ya Kati na Kusini na mwisho, Mweusi wa kutoka Afrika – mtoka mbali, nazo zimepitwa na wakati!

Tusisahau kuwa baadhi ya Weusi hao, wakereketwa wa u-Afrika, huwa wanajigamba na kuamini kuwa Seneta Barack Obama sio Mweusi-Halisi (Baba m-Afrika na Mama m-Amerika mwenye asili ya Ulaya)! Eti, hajui kula miguu ya nguruwe na mboga ya sukumawiki au kunywa uji (pigs feet and collard greens or grits) – chakula asili cha walalahoi Weusi wa Kusini ya Amerika! Hii inadhihirisha kuwa kuna pia ubaguzi miongoni mwa Weusi - wanabaguana!

Hata mpigania haki-mwenza wa Rev. Dr. Martin Luther King, Jr. (sasa mfanyabiashara mashuhuri na Mwenyekiti wa Goodwill International) Balozi wa zamani wa Amerika kwenye Umoja wa Mataifa na Meya wa zamani wa Jiji la Atlanta, Jimbo la Georgia, Andrew Young (mhudhuria mkuu wa Mikutano ya Sullivan), kwenye maoni ya toleo la TIME Magazine kabla ya kuapishwa kwa Rais-Mteule Barack Obama, alimtofautisha Bwana Barack Obama kwa kutokuwa na makovu ya kudhaliliwa au ya ulalahoi. Alikiri:

“(Obama) ni wetu, na tunamjivunia, lakini ukweli ni kwamba hana makovu ya uzoefu wa ulalahoi, kunyanyaswa na ubaguzi wa rangi ambao ulinikuza-ni vizuri kwake. Ana kitambulisho kisicho na makovu.” (Tafsiri ni yangu).

Weusi wengine waliufyata lakini baadaye, kwa sababu ya ki-historia, walibadili msimamo wao kufuatia kuteuliwa kwa Seneta Obama kuwa mgombea wa chama kimojawapo kikubwa.
BAP.

Swali la mjadala; je, Obama aliungwa mkono na weusi kwa sababu za kihistoria?

credit:mwanazuoni Born Again Pagan ( BAP)

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top