CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuendelea kushirikiana ili kuunda nguvu ya <endelea bofya kichwa cha habari hii juu>pamoja itakayosaidia kuharakisha maendeleo ya nchi kwa ufanisi zaidi.
Kimesema utendaji mzuri wa viongozi hao ndani ya Baraza hilo ndiyo utakaoweza kukirahisishia kazi Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa 2020, hali itakayojenga imani kwa wananchi kuirejesha tena CCM madarakati kutokana na utendaji mzuri wa viongozi hao.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Nd. Vuai Ali Vuai wakati akibadilishana mawazo na Katibu Mpya wa Kamati ya Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (Mnadhimu) huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini hapa.
Nd. Vuai alimpongeza kiongozi huyo kwa kuaminiwa na Wajumbe wa Baraza hilo na kumchagua kuwa Mnadhimu wa Wawakilishi wote wa CCM ndani ya Chombo hicho cha kutunga sheria za nchi.
Alisema kuchaguliwa kwa Mnadhimu huyo pamoja na msadizi wake kutasaidia kuongeza ufanisi wa kusimamia vyema shughuli za baraza la wawakilishi ili ziende sambamba na mahitaji ya wananchi majimboni.
Alieleza kwamba mbali na viongozi hao kuwa na jukumu la kuandaa miswaada, kutunga sheria na kupitisha Bajeti za nchi bado wana wajibu wa kusimamia kwa vitendo ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015/2020 pamoja na kulinda maslahi ya Chama hicho.
“Njia pekee ya kuepuka migongano na mivutano isiyokuwa ya lazima ndani ya Baraza la Wawakilishi ni lazima kila mara mkumbushane kufuata Kanuni na taratibu zilizopo ndani ya Chombo chenu.
Pia nyinyi ni kioo cha Wananchi waliokuchagueni kwa kura nyingi hivyo ni lazima muwawakilishe vyema na kuwa mifano mizuri ndani ya jamii kwani kufanya hivyo kutaongeza hamasa na ari ya watu wengi kuendelea kuiamini CCM.”, alisisitiza Vuai na kuongeza kwamba Uchaguzi umekwisha na kilichobaki kwa sasa ni kila kiongozi kufanya kazi za kuiletea nchi maendeleo endelevu.
Aidha Aliwataka Wajumbe wa Baraza la hilo kuwa na msimamo imara na kutokubali kuondoshwa katika Malengo kwani kuna njama na mikakati michafu inayofanywa na Viongozi wa CUF Zanzibar wenye nia ya kuharibu Haiba ya Chama na Serikali kwa ujumla.
“Juzi nimesoma katika baadhi ya magazeti kwamba CUF wana mipango ya kuishtaki serikali katika Mahakama za Kimataifa na wamezindua kitambu cha Ripoti ya Haki za Binadamu, hizo zote ni njama za siasa zilizopitwa na wakati za kutaka kukuondosheni katika malengo yenu na msikubali kuyumbishwa.”, alisema Vuai na kuwataka wawakilishi wasihofu juu ya Propaganda za CUF .
Aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati wote watakapohitaji ushauri na mawazo katika shughuli mbali mbali za Chama na Serikali .
Mapema akizungumza Katibu wa Kamati ya Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar(Mnadhimu), Ali Salum Haji alisema lengo la kikao hicho ni kujitambulisha kwa CCM na kupata nasaha, mawazo na ushauri mbali mbali wa kiutendaji kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu huyo ili waweze kuufanyia kazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Salum alieleza kwamba wana nia ya kuhakikisha ndani ya miaka mitano Bazara hilo linakuwa na mabadiliko makubwa yatakayopelekea wajumbe wake sio tu kufanya kazi za vikao bali wafanye utafti na kutembelea majimboni ili kubaini changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Naye Katibu Mndhimu Msaidizi, Nassor Salim Jazira, aliahidi kuzifanyia kazi nasaha na ushauri uliotolewa na Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai ili waweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika majimbo na Baraza hilo.
Alisema changamoto na vikwazo vya kisiasa vinavyotengenezwa na CUF toka kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Marudio havitoweza kupunguza kasi ya mabadiliko ya kimaendeleo yanayofanywa na Wajumbe wa Baraza, viongozi wa Chama na serikali kwa ujumla.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)