Takukuru Singida yamtia mbaroni Gulamali ( Aliyeshinda kura za Maoni CCM Jimbo la Nyalandu )


Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida inamshikilia mshindi wa kwanza kura za maoni CCM jimbo la Singida kaskazini, Haider Hussein Ghulamali (46), kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili taslimu kwa afisa usalama wa taifa (jina tunalo).


Lengo la Ghulamali mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha magodoro mjini Dodoma,ni kwamba afisa usalama huyo amtolee taarifa nzuri Kwenye vikao vya ngazi za juu, ili aweze kuthibitishwa na vikao hivyo, kuwa mgombea ubunge jimbo la Singida kaskazini.


Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, alisema Ghulamali amekamatwa Desemba 12 mwaka huu saa 8.30 mchana, maeneo ya Rafiki resort wakati akikabidhi rushwa hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kwenye bahasha.


Msuya alisema desemba 11 mwaka huu,ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwa mmoja wa wana CCM anayewania ubunge jimbo la Singida, ambaye ni Ghulamali.


“Baada ya kupokea taarifa hiyo uchunguzi ulianza ikiwa ni pamoja na kuchunguza vitendo rushwa alivyofanya mtuhumiwa huyo, kabla na baada ya kura za maoni kupigwa desemba 10 mwaka huu huko kijiji cha Ilongero.Kura hizo zilimpitisha Ghulamali aliyepata kura 606 kati ya kura 1009 zilizopigwa,” alisema.


Mkuu huyo, alisema baada ya zoezi hilo kupita la kura za maoni,mtuhumiwa kwa juhudi zake aliweza kupata namba za simu za afisa wa usalama wa taifa ambaye walikuwa hawafahamiani.


“Baada kupata namba ya simu ya afisa usalama taifa, Ghulamali aliweza kumpigia na akatoa maombi yake ya kusafishiwa taarifa kwenye vikao vya juu.Baada ya maombi hayo,aliweza kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili,na kumkabidhi afisa huyo. Ndipo alipokamatwa na TAKUKURU waliokuwa wameweka mtengo,” alisema Msuya.


Alisema uchunguzi zaidi bado unaendelea kuhusiana na mtuhumiwa Ghulamali kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wa kura za maoni.


Mkuu huyo wa TAKUKURU,ametoa rai kwa wanachama wa vyama vyote vya siasa,wagombea na wananchi kwa ujumla, kuzingatia sheria za uchaguzi ndani ya vyama vyao.Pia kujiepusha na vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi ndani vyama.


“TAKUKURU itamkamata mgombea,mpambe na mwanachama yeyote atakayejihusisha na vitendo ya kuomba na kupokea rushwa,na ikipata ushahidi wa kutosha,itamfikisha mhusika mahakamani,” alisema Msuya.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top