Wanawake Waongoza Kuwa Na Virusi Vya Ukimwi Nchini

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Utafiti wa Viashiria vya Virusi vya UKIMWI (VVU) na Maralia (THMIS) wa mwaka 2011/2012 kwa upande wa Tanzania Bara vinaonyesha kuwa idadi kubwa ya wanawake wameambukizwa ugonjwa huo kuliko wanaume.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alisema takwimu zilizopo sasa zinaonyesha kuwa asilimia 6.2 ya wanawake wameambukizwa ugonjwa wa ukimwi ikilinganisha na asilimia 3.8 ya wanaume.


Waziri Mhagama alisema kuwa kutokana na utafiti huo, maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na inakadiriwa kuwa jumla ya watanzania 1,538,382 wanaishi na VVU ambapo vijana wenye umri kati ya 15-24 ni asilimia 10.6 na watoto walio chini ya miaka 15 ni 11.8.


“UKIMWI bado ni janga kubwa nchini Tanzania kwani takwimu zinaonyesha kuwa maambukizo mapya yanakadiriwa kufikia watu 48,000 kwa mwaka hali ambayo inaashiria kupoteza nguvu kazi kubwa katika nchi yetu”


Kwa mujibu wa Waziri Mhagama alisema Tanzania itendelea kushirikiana na nchi nyingine Duniani kuhakikisha wanatokomeza janga la ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.


Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuwahamisha wananchi waendelee kujitokeza kupima afya zao ili wajitambue na kujua namna ya kujilinda kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza nchi wanachama kuwaanzishia dawa mara moja watu wote watakaopima na kugundulika kuwa na VVU.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dr. Leonard Maboko alisema kuwa kwa mwaka 2015 walioambukizwa VVU walikuwa Watanzania 2,100,000 ambayo ni idadi kubwa ukilinganisha na idadi ya sasa lakini pamoja na kushuka kwa idadi hiyo wananchi wanatakiwa kuendelea kujilinda mara dufu.


”Ingawa maambukizi ya VVU yameshuka kutoka Watanzania 2,100,000 hadi 1,538,382, Watanzania hatutakiwi kubweteka bali tunatakiwa tufanye jitihada za pamoja kuhakikisha janga hili linafikia mwisho,”alisema Dr. Maboko.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top