Rais wa Zanzibar Dkt Shein asema hamuogopi Maalim Seif, atoa ujumbe mzito

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna kiongozi yeyote wa kisissa nchini anayemuogopa.

Aidha, Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar ameahidi kumchukulia hatua yeyote atakayevunja sheria za nchi.

Amesema kuna baadhi ya wananchi, hasa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye amekuwa akivunja sheria za nchi kwa makusudi huku akijisifu na kuona kama serikali inamuogopa jambo ambalo sio sahihi.

Makamu Mwenyekiti huyo alitoa msimamo huo wakati akizungumza na mamia ya viongozi wa CCM, wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti na Makatibu wa Matawi na Maskani za Wilaya ya Mfenesini Kichama.

Mkutano huo ulifanyika katika Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Bububu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Dk. Shein alisema Zanzibar ina Rais mmoja ambaye ni yeye na kama kuna watu wanatamani nafasi hiyo ni lazima wachaguliwe kihalali.

Alikemea tabia za Maalim Seif ya kujaribu kila mara kuingiza nchi katika machafuko na aliahidi kuwa vyombo vya dola havitavumilia.

Alisema tayari dola inaendelea na taratibu za kisheria na endapo akitiwa hatiani atahukumiwa kisheria.

Maalim Seif alihojiwa na Polisi kwa saa tatu katikati ya wiki kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili.

“Mimi simuogopi Maalim Seif kwani ni kiongozi wa kisiasa kama mimi, ila tofauti yetu ni kwamba mimi ni Rais wa Zanzibar na yeye ni kiongozi wa chama," alisema na kueleza "hivyo haniwezi kwa lolote."

"Kwa mambo anayofanya, endapo akishitakiwa na kutiwa hatiani ajue kwamba kisheria kosa lolote la jinai halifi na wakati wowote anaweza kukamatwa na kushitakiwa endapo mahakama ikiona kuna haja ya kufanya hivyo."

Dk. Shein alisema Maalim Seif hawezi kuogopwa kwani hana vifaru, roketi renja za kivita vya kuwatisha watu wamuogope.

Alisema sheria ndio kinga dhidi ya migogoro ya Zanzibar na kiongozi yeyote atakayejifanya mbabe, hata akiwa rais wa nchi, sheria zitamshughulikia.

Aliwaambia wananchi wa Zanzibar wanaoona Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inavunjwa ama inataka kuvunjwa, wana haki ya kufungua mashtaka Mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 25 1(a).

Aidha aliahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 hadi ifikie asilimia 90 ili wananchi waendelee kupata maendeleo kwa wakati.

Dk. Shein alisema ahadi hiyo itatekelezwa kwa wakati endapo wananchi wataendelea kushirikiana vizuri na serikali katika shughuli na harakati mbali mbali za maendeleo ya nchi.

Rais shein alifafanua kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, CCM Zanzibar imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/2015 kwa asilimia 80.

Alisema kwamba mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya wananchi na viongozi mbali mbali wa Chama na serikali kwenye kuharakisha maendeleo ya nchi.

Aidha aliwapongeza wafuasi wa CCM katika Wilaya hiyo kwa kuichagua kwa kura nyingi CCM, katika Uchaguzi wa Marudio wa Machi 20 na kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 90.

Alisema kwamba ushindi huo ni taswira ya mafanikio ya Chama na serikali katika kuwatumikia wananchi kwa uadilifu mkubwa huku ikijipanga kuimarisha uchumi wa nchi kufikia uchumi wa kati.

“Uchaguzi Mkuu umekwisha hivyo kwa sasa tufanye kazi kwa pamoja kuendeleza maendeleo ya Zanzibar kwani kila jambo lenye tija na manufaa linahitaji umoja na ushirikiano kutoka kwa wananchi,” alisema Dk. Shein na kuongeza:

“Pia nakuombeni wafuasi wa CCM muendelee kuwa wavumilivu licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kisiasa kutoka kwa wapinzani.

"Jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi na vyombo vya kisheria." 

Dk. Shein alisema ataendelea kusimamia Sheria na Katiba ya Zanzibar kwa misingi ya uadilifu, lakini hatawavumilia watu wanaovunja sheria kwa makusudi.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top