Familia za Watu 8 Waliouawa Kwa Kuchinjwa Tanga Kujengewa Nyumba

Wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Tanga wameahidi kujenga nyumba nne kwa ajili ya makazi ya kaya ambazo ndugu zao waliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana katika kitongoji cha Kibatini, Jumanne ya wiki iliyopita.


Wakazi hao walihamia katika eneo la Kona Z baada ya ndugu zao wanane kuchinjwa na watu hao katika tukio linaloonekana kama kulipiza kisasi baada ya wakazi hao kuwaripoti polisi watoto wanane walioonekana kwenye kitongoji chao na kutiliwa shaka.


Wabunge waliahidi kujenga nyumba hizo baada ya kukuta familia hizo zikiishi katika mazingira magumu kwenye makazi yao mapya huku vyombo vyao vikihifadhiwa uwanjani.


Walitoa ahadi hiyo jana walipokwenda kutoa rambirambi kwa familia hizo.


Wabunge hao wote wakiwa wa CCM ni Adadi Rajabu wa Muheza, Jumaa Awesso na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.


“Hii haiwezekani, binadamu hawezi kuishi katika mazingira kama haya, hawa wananchi wapo katika machungu ya kufiwa, inatia simanzi kuona wamehamia huku, lakini hawana pa kuishi,” alisema Ummy ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu.


Alisema wabunge wa mkoa wa Tanga kupitia CCM watajenga nyumba nne Kona Z kwa ajili ya familia hizo, wakiwamo ndugu watatu wa familia moja ya marehemu Issa Hussein aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji.


“Tumekubaliana kwamba ujenzi huu utaanza mara moja wiki ijayo na tunataka nyumba zikamilike haraka ili wafiwa hawa waondokane na adha ya kukosa makazi,” alisema Awesso ambaye ni Mbunge wa Pangani.


Awesso aliitaka Serikali kuhakikisha inalinda maisha ya wakazi wa maeneo hayo pamoja na kufanya uchunguzi utakaowezesha kuwanasa walioshiriki mauaji hayo.


Wafiwa hao waliwaomba wabunge kuvishinikiza vyombo vya ulinzi na usalama kuweka ulinzi katika eneo hilo ili wasichinjwe watu wengine kwa kuwa bado wana hofu kwamba wanaweza kufuatwa.


“Kama mnavyoona tumekuja huku sisi kama tulivyo, tumeacha kila kitu Kibatini, mazao mashambani na mifugo tumeamua kukimbia ili kuokoa maisha yetu kwa hivyo tunakabiliwa na ukosefu wa chakula,” alisema Mwanaisha Hassan.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top