Samia ahimiza Superdoll kuwekeza katika kilimo



MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameitaka kampuni ya Superdoll kuendeleza uwekezaji katika maeneo ya ukanda wa kilimo. Samia alisema hayo juzi kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha huduma za magari cha kisasa cha Superdoll na matairi ya BF Goodrich KO2 mjini Arusha.

Alisema maeneo ya ukanda wa kilimo, yana changamoto ya barabara, kama ilivyo kwa barabara za mbugani, hivyo kufanya uwekezaji wa huduma hizo kutasaidia kupunguza gharama ya matengenezo ya magari. “Jitihada hizi zisiishie tu kwenye sekta ya utalii.

Tuna masuala ya kilimo, ule ukanda wa kusini mwa Tanzania, kuanzia mikoa ya Morogoro hadi Ruvuma, magari mengi sana yatakuwepo kule ukanda huu wa SAGGOT. Ardhi ni ile ile, kituo kama hiki kinahitajika kiwepo kule...kama kutakuwa na matatizo mengine kama ardhi, serikali itashirikiana nanyi,” alisema Makamu wa Rais.

Alieleza kufarijika kwake kwa kampuni hiyo, kuendelea kushirikiana na kampuni ya matairi ya Michelin kwa kuwapatia wateja bidhaa bora, zitakazowezesha kuwa kichocheo cha kuboresha huduma zao kwenye sekta ya utalii na kuvutia watalii wengi zaidi nchini.

Makamu wa Rais aliipongeza kampuni ya Superdoll kwa kazi kubwa wanayoifanya, ambayo inaongeza thamani kwenye sekta ya utalii na kusema mpango wao wa kujenga chuo, utaongeza ajira na pia ujuzi na thamani kwa vijana watakaotoka vyuo vya ufundi stadi (VETA).

Mapema, Mkurugenzi wa Superdoll, Seif Ali alimweleza Makamu wa Rais kuwa kampuni yake ilifanya uwekezaji huo kwa lengo la kukuza viwango vya usalama barabarani na hivyo kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.

Alisema Kampuni ya Superdoll, wasambazaji wa matairi nchini imezindua kwa mara nyingine tairi la BF Goodrich KO2 baada ya kufanya utafiti uliochukua miezi 18 kwa kushirikiana na Kampuni ya Michelin kuangalia namna ya kuboresha na kupata tairi mpya na imara na kutatua tatizo sugu la kupata matairi yenye kuweza kuhimili changamoto ya barabara za mbugani.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top