Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One) Dar es salaam.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Mei, 2016 alipofanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo na kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maafisa wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere waliokuwa wakitoa maelezo juu ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo, walikuwa wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi, hali iliyosababisha Dkt. Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa huwezi ukajiuliza? eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi miwili."Dkt. Magufuli aliwahoji Maafisa wa uwanja wa ndege
“Kwa hiyo mizigo inayoingia humu huwa hamuikagui kwa namna yoyote ile, kwa hiyo mtu nikiamua kuja na madawa yangu ya kulevya, nikaja na dhahabu zangu, na almasi zangu na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu” Rais Magufuli aliendelea kuwabana maafisa hao wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara hii ya kushtukiza mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akitokea Jijini Kampala nchini Uganda ambako jana alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)