Lipumba Amvaa Rais Magufuli.....Asema Vitisho Vitaangamiza Uchumi wa Taifa, Ampigia Hesabu za Kiuchumi Duniani Kuhusu Sukari

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuchoshwa na utendaji wa Rais John Magufuli katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi.


Prof. Lipumba alitoa kauli hiyo jana mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya CUF iliyopo Buguruni, Dar es Salaam.


Katika kukabiliana na changamoto za nchi hususani sekta ya uchumi, Prof. Lipumba amemshauri Rais Magufuli kutafuta ushauri sambamba na taratibu za kujenga uchumi wa soko shirikishi kutoka kwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu.


Alisema, uzoefu wa Rais Mkapa wa kujenga utawala wa serikali unaweza kumsaidia kufanya uamuzi sahihi utakayosaidia wananchi badala ya kukagandamiza.


Mchumi huyo alieleza kuwa, vitisho na ubabe wa Rais Magufuli vinaweza kuwaogopesha watendaji wake wakiwemo mawaziri na hivyo kushindwa kumueleza hali halisi na kwamba, kitendo hicho kinaweza kuathiri maendeleo ya nchi.


“Kuna dalili kwa baadhi ya watendaji wa serikali hasa mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya za kushindwa kutoa fikra zao zenye lengo la kuimarisha uchumi wa nchi au kueleza hali halisi iliyopo kwa kuhofia vitisho vya rais ili wasitumbuliwe,” amesema.


Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo wakati nchi ikiwa kwenye sintofahamu ya upatikanaji wa sukari ambapo kwa mujibu wake (Lipumba), uhaba huo umesababishwa na agizo la rais la kuzuia uingizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.


“Agizo alilolitoa Rais Magufuli Februari 28, 2016 wakati akiwashukuru waandishi wa habari, wasanii na makundi yaliyoshiriki kwenye kampeni zake za uchaguzi 2015 ndilo lililosababisha haya,” alisema na kuongeza;


“Kauli ya serikali ya kuzuia utolewaji wa vibali vya uingizwa wa sukari kutoka nje ndiyo iliyosababisha upungufu wa sukari, asiuaminishe umma kuwa sababu ni wafanyabiashara kuficha sukari.


“Kwa mwenendo huu nchi haitaendelea kutokana na kwamba badala ya vyombo vya dola kushughulikia masuala ya msingi ili kuleta tija katika maendeleo ya Taifa, vinahaha kutafuta sukari zilizofichwa.”


Alitoa mfano wa kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) cha kutafuta wafanyabiashara wanaoficha sukari badala ya kushughulika na masuala nyeti ya ubadhilifu wa mali za umaa kama Tegeta Escrow.


“Wafanyabiashara wanaopata kibali na wanaopitisha sukari kwa magendo wanapata faida kubwa kwa sababu bei ya sukari katika soko la dunia mwezi Agosti 2015 ilikuwa Dola za Marekani 250 kwa tani moja,” amesema.


Alifafanua kuwa, kama dola moja ni sawa na Sh. 2000 tani moja ya sukari iliuzwa Sh. 500,000 sawa na Sh. 500 kwa kilo moja na kwamba, ukiongeza na gharama za usafiri kila kilo moja ya sukari itafika kwa Sh. 600.


“Wafanyabiashara wakubwa na wa kati wanaoingiza sukari nchini hupata faida kubwa ukilinganisha na viwanda vya ndani kutokana na kwamba, uzalishaji sukari viwandani unagharimu mtaji mkubwa na kupelekea bei kuwa kubwa na kusababisha kupoteza soko,” alisema.


Alishauri kuwa, kama serikali ina lengo la kulinda viwanda vya ndani ihakikishe inaanda mfumo wa mnada wa ugawaji wa leseni ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara na viwanda kupata leseni za kuingiza sukari inayotoka nje ili viwanda vipate masilahi pamoja na wafanyabiashara.


“Ingawa utolewaji wa vibali utaathiri viwanda vya ndani kutokana na kushindwa kushindana na wafanyabiashara, ni vema serikali ikatoa vibali kwa watu wote,” alisema.


Kama serikali inataka kujenga uchumi wa viwanda haina budi kutoa motisha kwa wawekezaji ili wavutiwe kuwekeza katika sekta zote nchini.


“Rais anahitaji aelewe uchumi wa soko shirikishi, awape nafasi wahusika, asifanye maamuzi kwenye mikutano ya siasa au hadhara,”alisema.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top