Wadau Wapinga TANESCO Kupandisha Bei ya Umeme




Wakati wadau wa umeme wa jijini Dar es salaam wakisubiri wiki ijayo kutoa maoni kuhusu pendekezo la Tanesco kuongeza bei ya umeme kwa asilimia 18.19, wenzao katika kanda nne wamepiga hatua hiyo.


Msimamo huo umetolea katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya ambako vikao vya kukusanya maoni ya wadau vimefanyika chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura).


Jijini Mwanza.
Maofisa wa Tanesco, juzi walijikuta kwenye wakati mgumu kujibu hoja za wadau wa Kanda ya Ziwa kuhusu kutaka kupandisha bei, miezi michache tangu ipunguze kwa asilimia 1.1.


Pia, wadau waliwabana maofisa hao kueleza ni kwa nini shirika hilo halikusanyi madeni sugu kutoka serikalini na taasisi za umma, badala yake inawabebesha mzigo watumiaji wa chini ambao hulipia huduma kabla.


Mwenyekiti wa Kamati ya Walaji wa Bidhaa zinazodhibitiwa na Ewura Mkoa wa Mwanza, Jerry Mwasa alisema Tanesco imekosa ubunifu kiutendaji licha ya taifa kujaliwa vyanzo vingi vya umeme ikiwamo gesi asilia, makaa ya mawe, upepo na joto ardhi.


“Ni aibu maofisa wa Tanesco kuja hapa kudai eti bei za umeme Tanzania ni nafuu kulinganisha na Kenya, Uganda na Rwanda ambao hawana gesi wala makaa ya mawe kama Tanzania,” alisema Mwasa.


Akiwasilisha maoni ya Baraza la Ushauri la Walaji (Ewura CCC), Kaimu Mwenyekiti wa baraza hilo, Thomas Mnunguli alihoji ukinyonga wa Tanesco ambayo Machi 4 iliahidi kupunguza bei ya umeme kwa asilimia 7.9 ifikapo mwakani, lakini ghafla imebadilika na kutaka kuipandisha kwa asilimia 18.19.


“Kwa maoni yetu, Ewura ikatae maombi haya, badala yake Tanesco waagizwe kutekeleza agizo la kuwasilisha mpango mkakati wa kuboresha huduma, kupunguza bei na kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa sugu ikiwamo serikali na taasisi za umma,” alisema Mnunguli.


Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Serikali (GCC), Amani Mafura alishauri upandishaji wa bei ya umeme ufanyike kwa awamu ili isiathiri mpango wa Serikali wa kujenga “Tanzania ya viwanda” wala juhudi za wananchi kujikwamua kiuchumi.


Mmoja wa wadau, Frank Zekenuka alisema: “Wakati wateja tunalipia nguzo ambayo hata hivyo inasalia kuwa mali ya Tanesco, bado shirika hili linadai kuelemewa gharama za usambazaji. Hiki ni kiini macho cha kutulainisha tukubali ombi la kupandisha bei.”


Katika kikao cha Kanda ya Kati kilichofanyika Dodoma, wadau walisema kiasi kinachotakiwa kupandishwa ni kikubwa na mwananchi wa kawaida hataweza kukimudu.


Mwakilishi wa Ewura-CCC, Erasto Kishe alisema badala ya shirika hilo kupandisha bei ya umeme, linatakiwa kushusha kwa kuwa shughuli zote za maendeleo zinahitaji nishati hiyo hivyo hatua hiyo itapandisha gharama za maisha.


“Baraza linashauri Tanesco ianze kuwakatia umeme wadaiwa wake sugu ili kulazimisha kulipa madeni yao pamoja na riba kama zilivyo kanuni zake.


Mjumbe wa GCC, Ezamo Mponde aliitaka Ewura iitake Tanesco kutoa maelezo ya kina kwa nini inataka kupandisha bei kwa kipindi cha mwaka mmoja tu tofauti na utaratibu uliopo wa kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu.


“Ukipandisha gharama za umeme ni wazi kila kitu kitapanda bei na kama sababu ni kupanda kwa gharama za uzalishaji pamoja na madeni mliyonayo ni bora kama mngeirudisha ile asilimia 1.1 ambayo mliipunguza Aprili kuliko kuongeza bei kwa asilimia 18.19 baada ya miezi saba tu,” alisema Mponde.


Huko Mbeya, Ewura CCC imeitaka Tanesco kuweka mipango madhubuti ya kukusanya mapato kutoka kwa wadaiwa sugu walipe pamoja na riba badala ya kutaka kuongeza bei.


Mjumbe wa baraza hilo, Julius Mwambeso alisema Tanesco inaweza kupata fedha nyingi kama itakuwa makini kukusanya madeni ya wateja 4,036 wanaodaiwa Sh3.2 bilioni na kubana matumizi ya vikao vya bodi ambavyo vinafanyika mara 49.


Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika alisema Serikali inatoa mchango wake kwa Tanesco ili iweze kuwapunguzia makali wananchi.


Alisema hategemei kuona ongezeko lolote la bei ya umeme kutokana na ukweli kwamba Serikali ingependa wananchi wapate unafuu zaidi.


Maoni ya Tanesco
Naibu Mkurugenzi Mkuu (Usafirishaji Umeme) wa Tanesco, Kahitwa Bishaija alisema shirika hilo limelazimika kuwasilisha ombi la kupandisha bei ili kumudu gharama za uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na kuboresha huduma kwa wateja.


Alisema licha ya uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kuongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 58 mwaka huu, huku matumizi ya mafuta mazito kuzalisha umeme yakibakia asilimia tano pekee kulinganisha na asilimia 19 ya zamani, bado shirika hilo linakabiliwa na hali ngumu kiuendeshaji kutokana na madeni.


Alisema deni la Tanesco limeongezeka kutoka Sh699.57 bilioni Desemba mwaka jana hadi Sh794.48 Septemba na kwamba licha ya kuongeza mapato hadi kufikia Sh1,042.5 bilioni kulinganisha na Sh995.3 bilioni za mwaka jana, inalazimika kutumia wastani ya asilimia 13 ya mapato yake kwa mwezi kununulia mafuta ya kuzalisha umeme.


Bishaija aliwaeleza wadau kuwa ukokotoaji wa bei mpya inayoombwa umezingatia gharama ya ufuaji umeme, usafirishaji, usambazaji, uchakavu na uendeshaji.


Mhandisi kutoka Tanesco, Sophia Mgonja alisema ongezeko hilo la bei linatokana na ukame ulioikumba nchi kutokana na mvua kutonyesha kwa kiwango kinachotakiwa na kwamba kina cha maji katika Bwawa la Mtera ni kidogo hivyo wasipofanya juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya kuzalishia umeme, kutakuwa na mgawo.


“Pia kama mnavyofahamu kuwa mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa umeshatabiri kuwa mwaka huu hakutakuwa na mvua za kutosha hivyo kama tusipofanya juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya kuzalishia umeme tunaweza kukwama huko mbeleni,” alisema Mgonja.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top