Umoja wa Ulaya (EU) Wasema Tanzania ina haki kutosaini Mkataba EPA kama Haijaridhika Nao

BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Roeland Van de Geer amesema Tanzania ina haki ya kuamua kutosaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara na Jumuiya ya Ulaya (EPA) hadi itakapojiridhisha manufaa yake.


Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu masuala mbalimbali pamoja na kujibu maswali ya wanahabari hao.


Akizungumzia suala la Tanzania kutosaini mkataba huo wa EPA, ambao nchi wanachama waliosaini hufanya biashara bila kutoza kodi, Balozi Van de Geer alisema ingawa wasiwasi wa Tanzania kuwa mkataba huo utadhoofisha juhudi za nchi za kufufua viwanda vyake, haoni kama kuna ushindani kwenye hilo.


“Ingawa sioni ushindani unaohofiwa na Tanzania kwenye soko la EPA, lakini uamuzi wake wa kutosaini ni haki yao na nisisitize kuwa ni vyema Tanzania isisaini mkataba wowote ambao wana mashaka nao hadi pale watakapojiridhisha umuhimu wake,” alisema Balozi Van de Geer.


Aliongeza ni vyema nchi ikachukua muda kujiridhisha badala ya kukimbilia kusaini, kwa sababu endapo baadaye wataona mkataba huo hauna manufaa na huku wameusaini, watasononeka hivyo ni vyema wakaupitia na kuona kama una maslahi kwao.


Awali, Septemba mwaka huu, Mwenyekiti wa EAC, Rais John Magufuli alisema viongozi wote kwa pamoja walikubaliana kupewa muda wa miezi mitatu ili Sekretarieti ya EAC iangalie na kupitia masharti ya EPA kabla ya kusaini ili kila mmoja afaidike.


Hata hivyo, katika jumuiya hiyo ya EAC, nchi ambazo tayari zimesaini mkataba huo ni Kenya, Rwanda na Uganda na nchi zilizobaki ni Tanzania na Burundi.


Rais Magufuli alisema katika kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo yanapaswa kuangaliwa kabla ya kufikia uamuzi kwa maslahi ya nchi na wananchi.


Mwenyekiti alitaja mambo ya kuangaliwa kuwa ni kwa namna gani nchi za EAC zitafaidika, njia gani itatumika kuzuia bidhaa za kilimo na kulinda wakulima, usawa, makusanyo yatokanayo na bidhaa zitakazoingizwa, Burundi itasainije huku ikiwa imewekewa vikwazo na EU, kujitoa kwa Uingereza EU na athari zake, kukosekana kipengele cha kuruhusu nchi nyingine kujihusisha na nchi za EAC kibiashara, kukosekana ushuru wa forodha na kipengele cha nchi kujitoa pale inapoona haijaridhika na mkataba.


Rais Magufuli alisema mkataba huo ukisainiwa kwa wakati huu, nchi wanachama zinaweza kuingia kwenye mtego mbaya.


Akizungumzia kujiondoa kwa Uingereza kwenye EU, Balozi Van de Geer alisema EU bado iko imara na umoja huo utaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi imara duniani.


Kuhusu kiwango cha biashara baina ya Umoja wa Ulaya na Tanzania kwa mwaka, Balozi Van de Geer alisema hivi sasa mauzo yamefikia dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka huku akimsifu Rais Magufuli kwa sera yake ya viwanda na kusema umoja huo unamuunga mkono.


Aidha, aliisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujitahidi kuendesha nchi kwa kutumia vyanzo vya mapato vya ndani kwa wingi, badala ya bajeti kutegemea wahisani wa nje.


“Tumeona juhudi za serikali kwenye suala la bajeti ya sasa utegemezi wa wahisani kutoka nje ni chini ya asilimia 15 ya bajeti, ukilinganisha na awali ambapo bajeti kwa asilimia 40 ilikuwa tegemezi kwa wahisani, tunaona mabadiliko, na hii inaifanya Tanzania kuondoka kwenye nchi za kundi masikini zaidi duniani,” alieleza. 
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top