Hatimaye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imemwachia huru Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56) baada ya upande wa Jamhuri kuomba kumuondolea kesi kushawishi na kuomba rushwa ya Sh.milioni 30.
Ndassa alikuwa anakabiliwa na shtaka la kushawishi na kuomba rushwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichesmi Mramba.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dennis Lekayo jana aliwasilisha maombi ya kumwondolea Ndassa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa.
Lekayo alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), ameona hana nia ya kuendelea na mashtaka yaliyopo mahakamani dhidi ya mshtakiwa chini ya kifungu cha 98 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Aidha kwa mujibu wa kifungu hicho kinampa mamlaka DPP ya kumwondolea mashtaka mtuhumiwa kabla ya kusikiliza ushahidi lakini anaweza kukamatwa na kushtakiwa upya.
Hakimu Nongwa alisema kwa kuwa upande wa Jamhuri umeomba kumwondolea mshtakiwa mashtaka na kwamba hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo, mahakama yake imekubali ombi hilo.
"Mahakama hii inamwachia mshtakiwa chini ya kifungu cha 98 (a) kama upande wa Jamhuri ulivyowasilisha maombi yao dhidi ya mshtakiwa" alisema Hakimu Nongwa.
Mapema mwaka huu, Mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka la kushawishi na kuomba rushwa ya Sh. milioni 30.
Katika kesi ya msingi, Lekayo alidai kuwa Machi 13, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, Ndassa aliomba rushwa Sh.milioni 30 kutoka kwa Mramba.
Ilidaiwa kuwa aliomba rushwa ili awashawishi wajumbe wenzake wa kamati hiyo watowe mapendekezo mazuri katika mahesabu ya fedha ya Tanesco kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Katika shitaka la pili, mwakilishi huyo wa wananchi siku ya tukio la kwanza pia aliomba rushwa ya huduma ya umeme kwa kumshawishi Mramba atowe huduma hiyo kwa ndugu wa mbunge huyo Matanga Mbushi,Richard Ndassa na rafiki wa ndugu yake Lameck Mahewa.
Mbunge huyo alikana mashitaka yake na alikuwa nje kwa dhamana.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)