MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), ameiambia Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kwamba alishinda uchaguzi wa ubunge uliofanyika mwaka jana.
Bulaya aliyasema hayo mahakamani hapo jana mjini Musoma kupitia kwa wakili wake, Tundu Lissu, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Noel Chocha, anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo yake iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen Wassira.
Katika utetezi wake baada ya kuapa, Bulaya alisema alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo baada ya taratibu zote ikiwamo kuhesabu kura, kukamilika.
Baada ya utetezi huo, malumbano ya sheria baina ya mawakili wa upande wa waleta maombi na wajibu maombi yaliibuka na kudumu kwa zaidi ya saa tatu.
Malumbano hayo yalianza baada ya Wakili wa Waleta maombi, Costantine Mutalemwa, kuiomba mahakama hiyo iondoe aya saba kati ya 11 zilizokuwa kwenye utetezi wa Bulaya kwa kile alichodai hazimo kwenye utaratibu wa awali uliowasilishwa mahakamani hapo.
Aya ya saba ya utetezi wa Bulaya inadai kasoro ya kura 164,794 zilizotangazwa awali na msimamizi wa uchaguzi badala ya kura 69,369 za wapiga kura halali, hazikuathiri matokeo.
Wakili Mutalemwa alidai kwamba, madai yaliyotokea kwenye utetezi wa mbunge huyo ni mapya na suala la idadi ya wapiga kura ni moja ya kipengele ambacho wateja wake wanakipinga.
“Naomba mheshimiwa jaji aya ya pili, tatu, nne, tano, sita, saba na nane, ziondolewe kwenye utetezi wa Bulaya na zibaki aya ya kwanza, ya tisa, ya 10 na aya ya 11.
“Naomba aya hizo ziondolewe kwa sababu ni mpya na hazipo kwenye utaratibu wa awali,” alidai Wakili Mutalemwa.
Kutokana na maombi hayo, Lissu alisema hakubaliani na pingamizi la wakili huyo.
Alisema amekumbuka kauli ya aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Mahakama ya Afrika Mashariki, Sir Charz Nyubon aliyewataka mawakili wasiweke mapingamizi yasiyo na msingi.
“Kitendo cha mawakili kuweka mapingamizi yasiyo na msingi ni kupoteza muda wa mahakama kwa mujibu wa kauli ya rais huyo na nakuomba mheshimiwa jaji uendelee na ushahidi wa mtoa ushahidi kwa kuwa muda wa kupoteza kwenye ushahidi haupo,” alisema Lissu.
Naye Wakili wa Serikali, Angela Lushagamba, alisema hana pingamizi lolote kwenye kiapo cha utetezi wa Bulaya uliotolewa mahakamani hapo na kuiomba mahakama iendelee kusikiliza ushahidi.
Akitoa uamuzi juu ya hoja zilizoibuka mahakamani hapo, Jaji Chocha, alisema anaona dalili za shauri hilo kusikilizwa kwa muda mrefu kutokana na hoja mpya zilizoibuka mahakamani.
“Kuna vitu vipya ambavyo vimeibuka kwa siku ya leo na nahitaji nipate muda zaidi ya saa tano kuvifanyia kazi,” alisema Jaji Chocha huku akiahirisha kesi hiyo hadi leo saa saba mchana.
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)