22 CUF wafikishwa mahakamani

Wakati wafuasi 22 wa CUF wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka manne, likiwamo la kumiliki vifaa vya Jeshi la Polisi kama mabomu ya machozi, Profesa Ibrahim Lipumba amepata upinzani mikoa ya Kusini.


Kamati ya Utendaji ya CUF wilayani Tandahimba ilikutana na mjumbe wa Baraza Kuu na kutoa tamko la pamoja kumpinga Profesa Lipumba, ambaye anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.


Mwenyekiti wa wilaya hiyo ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Katani Katani amesema wamekutana na kamati ya utendaji ya wilaya na kuunga mkono kwa dhati uamuzi wa Baraza Kuu wa kumfukuza uanachama Profesa Lipumba.


Walisema katiba ya CUF inaeleza vizuri katika sura ya pili kuhusu haki na wajibu wa mwanachama.


Kuhusu ziara ya kiongozi huyo mikoa ya Kanda ya Kusini, mwenyekiti wa Kata ya Litehu, Awadhi Nampanda alisema kitendo cha Profesa Lipumba kufanya ziara mkoani Mtwara na kuiruka Wilaya ya Tandahimba ni mwendelezo wa kukihujumu chama na kuwataka CUF nchi nzima kuendelea kumpinga. “Kwa kweli nasikitika sana taratibu hizi anazotumia Profesa Lipumba. Alitutosa, leo anarudi tena. Haheshimu katiba,” alisema.


“Sijui anaenda na katiba gani sasa. alifanya ziara mjini Mtwara akatupita hapa Tandahimba kwenda Newala. Naomba wanachama wote wa CUF nchi nzima wasikubaliane naye,” alisema Nampanda.


Jijini Dar es Salaam, wakili wa Serikali, Patrick Mwita alidai wakati akisoma mashtaka mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu jana kuwa wanachama hao 22 wa CUF na wenzao ambao hawakuwepo, walipanga njama za kuunda kikosi cha kufanya kazi na majukumu ya Jeshi la Polisi.


Alidai kuwa walipanga njama hizo kati ya Septemba 20 na 25 wakiwa maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar na Dar es Salaam.


Alidai kuwa waliunda kikosi cha “Blue Guards” kilichotwaa majukumu ya polisi kinyume cha Sheria ya Polisi na Huduma Saidizi.


Amedai kuwa kati ya Septemba 20 na 25, mwaka huu visiwani Zanzibar na Dar es Salaam, washtakiwa hao wakiwa wanakikundi wa Blue Guards walijiimarisha na kutwaa majukumu ya polisi na Septemba 25 walikamatwa wakiwa na visu 10 na mabomu ya machozi maeneo ya Mwananyamala A wilayani Kinondoni kwa nia ya kutenda uhalifu.


Amewataja washtakiwa hao kuwa ni Said Omary, Said Mohamed, Hamid Humudi, Othuman Hamad, Swalehe Ally, Hamis Haji na Majid Juma.


Wengine ni Mohamed Ally, Ramadhan Rashid, Juma Hamad, Masoud Fumu, Jecha Faki, Mbaruku Bakari, Mohamed Zuberi, Muhsin Juma, Mohamed Amir, Ally Juma, Ally Nassoro, Haji Juma na Juma Hamis.


Wakili Mwita alidai kuwa vifaa walivyokutwa navyo Kinondoni hutumiwa Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao.


Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika.


Upande wa utetezi uliiomba mahakama ufute shtaka la tatu kwa madai kuwa lina upungufu wa kisheria na halikidhi matakwa ya kisheria.


Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top