Na Mwl Joseph b Maduka.
Maisha yanaongozwa na Kanuni, ukikosea Kanuni hizo umekosea maisha.
Kila unachofanya kina matokeo yake, Psychology inasema 'Law of cause and effect' ikiwa ina maana matokeo ya jambo lolote lile linategemea na chanzo /msingi wake.
Biblia inasema kile upandacho ndicho utakachovuna, haijalishi utapita muda gani ili mradi ulipanda basi kuvuna ni lazima. Sasa itategemea ulipanda nini.
Kuna watu wapo kwenye maumivu na majeraha makubwa ya Nafsi kutokana na kuumizwa Katika mapenzi.
Lakini maumivu hayo ni matokeo ya kile walichopanda Katika hayo mahusiano yao, hivyo maumivu ni mavuno yao wanayostahili.
Watu wengi sasa hawana subira, hawataki kufuata utaratibu, wamekuwa na kihele-hele kisichokuwa na maana.
Unakuta watu wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi huu tu wa kawaida, tayar wameshaanza kuishi maisha kama vile wanandoa.
Tayari wameshaanza kushiriki tendo la ndoa, wameanza kufanya biashara kwa pamoja, kununua viwanja kwa pamoja, kujenga na mambo mengi kama hayo.
Sasa huwa najiuliza, wanapofanya mambo hayo wana UHAKIKA gani kama Kweli watafunga ndoa? Itakuwaje inapotokea wameachana na tayar wameshafanya mambo yote hayo?
Kuna wengine wamewalipia gharama na kuwasomesha wapenzi wao na kuishiwa kuachwa tena kwa dharau.
Sasa hapo ndio ile misemo ya sijui umenipotezea muda, umeniharibia maisha yangu, wanaume /wanawake wote ni matapeli, hujitokeza..!
Hapa ndipo nakumbuka ule msemo usemao 'Akili ni nywele, kila mtu ana zake'.. Wakati unayafanya yote hayo ulikuwa unategemea nini? Ulifikiri upo kwenye Ndoa? Au ndo ulikuwa unajitutumua uoenekane unajua kupenda?
Katika dunia hii ya sasa unaanzaje kufanya mambo ya kitoto kama hayo,Kweli mapenzi ni upofu. Kama ikiwa watu walio kwenye ndoa wanasalitiana sembuse wewe na huyo mtu wako ambaye isikute hata kwao hupajui mnaishia kuonana bar tu na Kwenye grocery.
Wakati unafanya hayo yote ulikuwa Katika wakati wa kucheka, lakin ukasahau kuna upande mwingine pia wa Kulia. Kama ungefahamu hili nadhan ungekuwa MAKINI Katika Maamuzi yako.
Sina maana watu wasisaidiane, La hasha..! Ila kama msaada basi utolewe kwa KIASI, acha moyo upande lakini Akili IAMUE.
Nimekutana na wadada waliojitoa kwa wanaume kupita kiasi zaidi hata ya mke anavyopaswa kuwa, walifanya Vitu vingi vya maendeleo na hao wanaume lakini waliishia kuachwa na kuolewa wengine.
Sasa wanaishi na vinyongo na wengine wanapanga hata Kulipiza KISASI.. Wamefika hatua hawaoni umuhimu na furuha tena ya maisha.
Ni waathirika wa mapenzi. Wasioasidika kwa dawa wala kwa ushauri, ni Mungu tu aingilie kati. Hata wanaume nao wapo waliotendwa. Hakuna upande uliosalimika.
Yote haya ni kwa sababu ya kushindwa kuzingatia KANUNI Katika swala la mahusiano.
Mambo ya urafiki yafanyike Katika urafiki, mambo ya uchumba yafanyike Katika uchumba, na mambo ya Ndoa yasubiriwe wakati wa Ndoa.
Hii ni Kanuni, ukiivunja, itakuvunja. Kila jambo na wakati wake. Ukicheka, kumbuka kuna Kulia.
♥PENDA MOYONI, AKILI KICHWANI..!
# UCHUMBA SIO NDOA..................
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)