Trump akereka mshukiwa wa New York kutibiwa na kupewa wakili

 
Bw Trump amesema inasikitisha kwamba Bw Rahami, ambaye ana uraia wa Marekani, atapokea matibabu na kupewa wakili

Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amelalamikia hali kwamba mshukiwa anayedaiwa kutekeleza shambulio New York Ahmad Khan Rahami alitibiwa baada ya kujeruhiwa wakati wa ufyatulianaji risasi na maafisa wa polisi Jumatatu.

Aidha, amekerwa na hali kwamba mshukiwa huyo bado atapewa wakili na serikali.

Mshukiwa huyo mzaliwa wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 28 amefunguliwa mashtaka matano ya kujaribu kutekeleza mauaji.

Bw Trump akihutubu Fort Myers, Florida amesema hiyo si "hali nzuri" na inaashiria mifumo dhaifu ya usalama wa taifa nchini Marekani.

"Jambo la kusikitisha, sasa tunampa huduma nzuri sana ya kimatibabu. Atatibiwa na baadhi ya madaktari bora zaidi duniani," Bw Trump alisema.


"Atapewa chumba cha kisasa hospitalini. Na labda atakuwa akipokea huduma zote akiwa humo humo chumbani, ukizingatia jinsi taifa hili lilivyo."

Mgombea huyo alidokeza kwamba hakuna adhabu yoyote ambayo inaweza kutosha kwa Bw Rahami.

"Ni hali ya kusikitisha sana," aliongeza.

Amerejea wito wake wa wahamiaji wanaoingia Marekani kutoka nje "kuchunguzwa kwa kina", ili miongoni mwa mengine, kubaini iwapo wanaamini katika maadili ya Kimarekani.

Hayo yakijiri, mpinzani wake kutoka chama cha Democratic Hillary Clinton amesema maneno ya Bw Trump yanasaidia tu makundi ya kigaidi.

"Matamshi haya na lugha ambayo Bw Trump anatumia vinasaidia na kuliwaza maadui zetu," Bi Clinton aliambia kikao cha wanahabari nje ya jiji la New York.

Bw Trump alijibu kupitia taarifa na kusema iwapo Clinton atakuwa rais, basi "mashambulio zaidi yatatekelezwa hapa nyumbani na Wamarekani wengine wengi wasiokuwa na hatia wataumizwa na kuuawa."

Tuyajuayo kufikia sasa:
Ahmad Kham Rahami alikamatwa kuhusiana na milipuko ya New York na New Jersey
Ni raia wa Marekani mzaliwa wa Afghanistan
Anakabiliwa na mashtaka matano ya kujaribu kuwaua maafisa wa polisi, lakini hakuna mashtaka yoyote yanayohusiana na ulipuaji kufikia sasa

Tusiyoyafahamu kufikia sasa:
Lengo la mashambulio hayo na iwapo alikuwa na itikadi kali
Iwapo ana uhusiano na kundi linalojiita Islamic State
Jinsi maafisa walivyomtambua Bw Rahami kuwa mshukiwa mkuu
Watu 29 walijeruhiwa kwenye mlipuko uliotokea mtaa wa Chelsea, New York. Kilipuzi ambacho hakikuwa kimelipuka kilipatikana hapo karibu.

Vilipuzi vingine kadha vilikuwa vimepatikana New Jersey siku za hivi karibuni.
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top