WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amevitaka viwanda vya sukari nchini kuongeza mikakati ya uzalishaji zaidi ili mwaka 2020 Tanzania iwe imefikia kiwango cha kuzalisha asilimia 100 ya mahitaji
yake.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Agosti 02, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha sukari cha Mtibwa kilichoko mkoani Morogoro ambapo amesisitiza viwanda vya ndani vizalishe zaidi ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
Amesema Serikali imejikita katika kuimarisha na kulinda viwanda vya ndani nchini hivyo ni vema viwanda vya sukari vikaweka mikakati ya kuzalisha kwa wingi ili kuondokana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje.
“Kiwango cha mahitaji ya sukari nchini ni zaidi ya tani 400,000, nimeiagiza Bodi ya Sukari kukaa na wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kufanya utafiti ili tujue mahitaji halisi ya sukari,” alisema.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mkakati wa kulinda viwanda vya ndani kwa kuziongezea kodi bidhaa zinazotoka nje ambazo zinazalishwa na viwanda vya ndani ikiwemo sukari hivyo wenye viwanda hawana budi kuzalisha kwa wingi zaidi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa viwanda vya sukari nchini kutoa motisha kwa wakulima wa nje kwa kununua miwa yao kwa bei nzuri na kuwalipa kwa wakati ili nao wanufaike na uwepo wa viwanda hivyo na kuwa walinzi wa uwekezaji huo.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano Mwandamizi wa kiwanda hicho, Ibrahim Juma amesema kwa sasa kiwanda kinazalisha tani 20,000 kwa mwaka na wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 70,000 ifikapo mwaka 2021.
Juma alisema uzalishaji wa sukari kiwandani hapo ulipungua kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje hivyo aliipongeza serikali kwa kudhibiti uingizwaji holela wa sukari kutoka nje jambo litakalosaidia ukuzaji wa viwanda vya ndani.
Meneja huyo alisema kuwa kwa sasa wameanza upanuzi wa mashamba kiwandani hapo ambapo wanatarajia kuongeza hekta 400,000 lengo likiwa ni kutimiza ndoto ya Serikali ya kuifanya Tanzania ijitosheleze katika uzalishaji wa sukari.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 02, 2016.
Bilionea wa Chadema Akitosa Chama Hicho, Aahidi Kutoa Trilioni 10 za Kuwekeza Dodoma ili Kumuunga Mkono Rais Magufuli bofya hapa
HABARI KUU LEO BOFYA HAPA
Post a Comment
Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)