Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa agundua Ufisadi wa Kutisha soko la Mwanjelwa, Amuagiza CAG Afanye Ukaguzi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya baada ya kuwepo kwa ubadhilifu katika ujenzi wa soko la Mwanjelwa
.


“Inasikitisha ujenzi wa soko hili kuingia ubabaishaji. Ujenzi wa soko ungegharimu sh bilioni 16 ila sasa watendaji wamefanya mambo ya hovyo na kufikia sh bilioni 26 hatuwezi kuwavumilia lazima hatua zichukuliwe kwa wote watakaobainika katika ubadhilifu huu,” alisema.

Pia amempa siku tatu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla kufanya uchunguzi na kubaini nani aliyetafuna sh milioni 489 zilizotolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya uendelezaji wa soko hilo ambazo hazijulikani zilipo.


Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 09, 2016) wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika soko la Mwanjelwa na kubaini ubadhilifu wa fedha katika ujenzi wa soko hilo.


Waziri Mkuu amesema mara baada ya CAG kumaliza kufanya ukaguzi atatoa taarifa na mtu yeyote atakayetajwa katika ripoti hiyo kuwa amehusika na ubadhilifu huo atawajibika hata kama yuko nje ya Jiji la Mbeya.


Alisema kitendo cha kuongeza gharama za ujenzi wa soko hilo kutokana na kuchelewa kwa ujenzi wake kinaisababishia Halmashauri yaJiji kulipa sh milioni 200 kila mwezi kwa ajili ya marejesho, hivyo aliagiza aliyesababisha gharama hizo asakwe na achukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.


Wakati huo huo Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa Mkoa Mbeya, Amos Makalla kuhakikisha mtu aliyepangishwa katika kibanda cha kukusanyia uchafu sokoni hapo anaondolewa haraka na kurudishiwa fedha zake ili kibanda hicho kitumike kama ilivyokusudiwa.


Pia alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kufanya ukaguzi katika vyumba vya maduka sokoni hapo na ifikapo Jumatatu mtu hajaweka mali anyang’anywe na kupangishwa kwa mtu mwingine mwenye kuhitaji.


Alisema hayo baada ya baadhi ya wafanyabiashara kulalamika kuwa kuna watu wamechukua vyumba vingi vya maduka kwa ajili ya kuvipangisha kwa wafanyabiashara kwa gharama kubwa tofauti na inayotozwa na Halmashauri, hivyo kunyima nafasi kwa walengwa kunufaika na soko hilo.


Mmoja wa wajasiriliamali sokoni hapo Mohammed Said alisema watu wameshika vyumba na kuviuza kwa sh milioni 20 hadi 40 kulingana na eneo kilipo chumba jambo linalosababisha baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kupata nafasi katika soko hilo.


Awali Mkuu wa Mkoa alisema soko hilo linakabiliwa na matatizo mbalimbali kwani hata wahanga waliokuwa wanafanya biashara kabla ya soko kuungua moto hawakupewa kipaumbele wakati wa upangishaji wa vyumba vya maduka.


Kuhusu suala la kukosekana kwa wateja sokoni hapo Makalla amewataka wafanyabiashara wote wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyokuwa rasmi kuhamia sokoni hapo mara moja.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 08, 2016.


Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top