Vyuo Vya Udereva Visivyo Na Sifa Mbioni Kufungwa

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema litavifungia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya udereva nchini bila ya kuwa na sifa.

Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishina wa Polisi (DCP) Mohamed Mpinga wakati akifungua mkutano wa pili wa Chama cha Shule Binafsi za Udereva Tanzania (Chashubuta) uliofanyika Dar es Salaam jana.


"Kuanzia sasa Jeshi la Polisi halitasita kukifungia chuo chochote cha udereva kitakachokosa sifa kwani kwa kulea shule mbovu tutaendelea kupata ajali na hivyo kuongeza vifo na majeruhi" alisema Mpinga.


Mpinga alisema kwa mujibu wa sheria ya shule za udereva sura 163 ya 1965 (R.E 2002) mpaka sasa jeshi la polisi limesajili shule za udereva 260 ambazo zitategemewa kutoa madereva bora wenye ueledi wa kutosha kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha ajali ni makosa ya kibinadamu ambayo yanafanywa na madereva.


Alisema jeshi hilo litafanya msako nchi nzima kuvibaini vyuo ambavyo havina sifa na wamiliki wake kuchukuliwa hatua na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.


Mwenyekiti wa Chashubuta Taifa, Robert Mkolla wakati akisoma risala yao mbele ya Mpinga ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mkutano huo, alisema moja ya changamoto waliyonayo ni baadhi ya wadau wa sekta ya usafiri na usafirishaji kutoona mchango mkubwa unaofanywa na shule za udereva za watu binafsi wakiamini kuwa vyuo vinavyotoa elimu nzuri ni vile vya serikali pekee.


Mkolla alimuomba Kamanda Mpinga uboreshwaji wa mitaala mara kwa mara ili kwenda na mahitaji ya barabara, vyombo na wakati na shule hizo ziwe zinashirikishwa katika kutoa michango ya uboreshaji wa mitaala hiyo.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top