Polisi yawatia mbaroni watu watatu waliojiunganishia umeme Kinyemela Jijini Mwanza



Watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilayani Ilemela kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyemela kwenye nyumba zao kinyume na utaratibu uliowekwa na TANESCO.


Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Mwanza imesema kuwa mnamo tarehe 31.07.2016 majira ya saa 5:10 asubuhi katika maeneo ya Ilemela Mlimani wilaya ya Ilemela jiji na mkoa wa Mwanza, watu watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyemela kwenye nyumba zao kinyume na sheria na utaratibu uliowekwa na TANESCO.


Imewataja watu hao kuwa ni Boniphace Masamaki miaka 47, Lina Cosmas miaka 26 na Ali Mohamed miaka 30 wote wakazi wa mtaa wa Ilemela Mlimani.


Aidha watuhumiwa hao waliweza kukamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa raia wema, ndipo jeshi la polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TANESCO waliweza kufanya msako maeneo hayo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.


Watuhumiwa wote wapo katika mahojiano na jeshi la polisi wakishirikiana na TANESCO, pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.


Msako wa kuwasaka watu wengine ambao wamejiunganishia umeme kinyume na utaratibu bado unaendelea.


Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza Naibu Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza akiwataka kuacha tabia ya kujiwekea umeme kinyemela katika nyumba zao kwani ni kosa la jinai lakini pia wanahatarisha maisha ya familia pamoja na mali zao.


Amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi wema na maofisa wa TANESCO litahakikisha linawasaka na kuwatia nguvuni watu wote wanaodaiwa kujiwekea umeme kinyemela kwenye nyumba zao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
 
 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top