Waziri wa Fedha Dr Philip Mpango Akemea Wanaopotosha Taarifa za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za utalii

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amekemea wanaopotosha taarifa za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za utalii.
Amesema kodi hiyo iliwekwa miaka miwili iliyopita; na serikali haina sababu ya kuwaongezea wananchi mzigo huo.


“Hata hao wanaosema utalii umepungua kwa sababu ya kodi hiyo, watoe hizo takwimu tuzione, watalii wanaangalia vitu vingi ikiwemo vivutio, usalama, amani, magonjwa. Wasiotaka kulipa kodi wanawachanganya tu wananchi...tunasisitiza kila mwananchi kulipa kodi. Tunachotaka sisi ni Taifa lifaidike na rasilimali ambazo Mungu ametupatia,” alisema Waziri Mpango.


Dk Mpango alisema hayo jana mjini Morogoro, wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha wakaguzi wa ndani wa wizara, idara, wakala, sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa, iliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).


Ufunguzi huo ulikwenda sambamba na uzinduzi wa miongozo mitatu ya ukaguzi wa ndani.


Pia, Waziri Mpango aliwataka watumishi wa umma, kufuata na kutekeleza maagizo ya serikali, ikiwa ni pamoja na kufanyia mikutano na semina zote katika kumbi za serikali.


Alisema vinginevyo watachukuliwa hatua kama vile kukatwa mishahara ili kufidia fedha za serikali wanazozitumia kulipia kumbi. Dk Mpango alisema agizo hilo linatakiwa kutekelezwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu ili kuokoa fedha za umma.


“Atakayekiuka hili tutamkata mshahara wake maana watoto wanakaa chini, hospitalini hakuna vitanda na magodoro, hakuna maji, hakuna madarasa, hakuna vyoo, hivyo tunatakiwa kupunguza matumizi ambayo si ya lazima ili tuboreshe sekta zingine,” alisema Dk Mpango.


Alisema hata kama semina au mkutano unagharamiwa na wafadhili, ni jukumu la viongozi wa umma kuwaomba kufanyia mikutano hiyo kwenye kumbi za serikali ili fedha zinazobaki zitumike kwa kazi nyingine. 


Aliwaagiza wakaguzi wa ndani kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa ili kudhibiti mchwa wanaotafuna mali za umma.


Alisema kuna hisia na madai kuhusu uadilifu mdogo wa baadhi ya wakaguzi wa ndani na hivyo kusababisha kushindwa kutoa taarifa za vitendo vya ubadhirifu kwa sababu nao ni sehemu ya washiriki wa vitendo hivyo.


“Natambua si wakaguzi wa ndani wote ambao uadilifu wao unatiliwa shaka. Nafahamu kwamba wapo waliowajibishwa kwa ajili hiyo. Hivyo naomba muongeze bidii katika mapambano haya na serikali hatutawaonea haya wakaguzi wachache wanaoendelea kuchafua jina la taaluma hii. Tutawachukulia hatua kali za kinidhamu wale wote watakaokwenda kinyume na taaluma hii,” alisema.


Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Toshio Nagase alisema Serikali ya Japan kupitia JICA imekuwa ikitoa msaada wa kitaalamu kwa Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani katika kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani tangu mwaka 2009.

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top