TCRA yaipiga Clouds Tv adhabu kwa Kurusha kipindi chenye maudhui ya ushoga.



MAMLAKA ya mawasiliano nchini (TCRA) imetoa onyo pamoja na kuutaka uongozi wa Clouds TV kuomba radhi Watanzania kupitia taarifa zake za habari ndani
ya siku tano mfululizo kuanzia jana.


Adhabu hiyo ilitolewa jana na kamati ya Maudhui ya TCRA, baada ya baadhi ya wananchi hususani watazamaji wa kipindi cha ‘Take One’ kilichorushwa 28 Juni mwaka huu ambacho kilidaiwa kueleza masuala ya mapenzi ya jinsia moja (Ushoga), kulalamikiwa kwamba kilikiuka maadili ya taifa.


Wakati akisoma tamko la adhabu hiyo, Joseph Mapunda, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya wajumbe wa kamati kutafakari maelezo ya utetezi yaliyotolewa na uongozi waClouds TV.


“Tumetafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na clouds tv kuhusu kipindi chake cha Take One kilichorushwa hewani tarehe 28 June 2016 ambacho kilikiuka baadhi ya kanuni za maadili ya utangazaji,” alisema Mapunda.


Aliongeza kuwa “kutokana na kipindi hicho kuwakwaza pamoja na kuwasababishia usumbufu wananchi hususan watazamaji kwa kuwasilisha mada inayozungumzia masuala ya mapenzi ya jinsia moja (ushoga), Clouds TV inatakiwa kuwaomba radhi watanzania wote na watazamaji.”


Alisema taarifa ya kuomba radhi itoke siku tano mfululizo katika taarifa zao za habari ya saa moja na nusu na ya saa tano usiku kuanzia siku ya kusomwa hukumu, na kwamba uthibitisho wa taarifa hizo upelekwe TCRA siku ya Jumatano tarehe 13 Julai 2016 kabla ya saa kumi jioni.


“ Hatua ya pili, Clouds Tv inatakiwa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha inazingatia kanuni zote za utangazaji nchini katika kutekeleza majukumu yake ya utangazaji,” alisema na kuongeza.


“Kamati inawaonya vikali Clouds tv kwa kukiuka kanuni za huduma za utangazaji (maudhui) ya mwaka 2005, namba 5(b), 5(c), 5(d) na 15(c) 16(2) uamuzi huu umetolewa leo, haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu iko wazi ndani ya siku 30 tangu siku uamuzi unapotolewa.


Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Clouds Media Group alisema baada ya kutafakari tamko la adhabu atatoa msimamo wake kama watakata rufaa au la.


“Tunaweza tukarudi nyuma na kusema tufanye kazi ya kukata rufaa, kwa sababu tunaamini na mimi nina simamia msimamo wangu kwamba tunapoambiwa tunalinda maadili ya kitaifa, kupinga jambo lolote baya ni kulinda maadili ya kitaifa,” alisema na kuongeza.


“Sasa ukiambiwa kwamba ulipinga kwa namna ya ulivyo pinga ni tofauti kidogo labda inaweza ikasaida kutengeneza mjadala mkubwa wa kujiuliza maadili tunayotakiwa kuyalinda ni yapi.”


Mutahaba alisema “Lakini moja kati ya kitu tunachokiona kina utofauti ni kuna baadhi ya mambo yamezungumzwa ambayo sikumbuki kabisa kama yako kwenye kipindi, kwa hiyo sijui wamezitolea wapi.”


Alisema kuwa ushoga ni tatizo na kwamba lazima alikemee na ataendelea kulikemea.


“Kwa ajili ya kosa la kutaja neno shoga katika kipindi cha njia panda mwaka 2000, miaka minne iliyopita kwenye gazeti tulivyosoma neno ushoga tukatozwa faini ya mil 5, haiwezekani miaka kumi na sita inapita kutaja neno shoga kila siku mtu anapewa adhabu,” alisema

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top