Mke Ambwaga mkwewe kortini Katika Kesi ya Kugombea Sehemu ya Kumzika Marehemu Mumewe


Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imeyatupilia mbali maombi ya kuzikwa Tanga mwili wa Andrew Daffa, aliyefariki dunia Jumatano iliyopita katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam
Mwili wa Daffa ulizuiwa kuzikwa kutokana na maombi ya kesi ya madai namba 240 ya mwaka 2016, yaliyofunguliwa na baba yake, Charles Joseph ambaye alitaka apewe kibali cha kumzika mwanaye Kijiji cha Vigiri mkoani Tanga alikozaliwa. 


Mvutano huo ulijitokeza baada ya mke wa marehemu, Glory Charles kutaka kupewa haki ya kuzika mwili wa mumewe katika makaburi ya Kwa Jimmy yaliyopo Yombo Vituka. 


Glory aliieleza Mahakama kuwa eneo hilo ndilo walilozika watoto wao watano, ambao alizaa na mumewe. 


“Kwa sababu mume wangu alikuwa anaishi na mimi Tabata Kimanga na nilimuuguza mpaka dakika ya mwisho bila kupata msaada wa ndugu yeyote, naomba Mahakama inipe kibali cha kumzika kwani na mimi nina haki kama mke,” alidai Glory, 


Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Adelf Sachore alisema Mahakama inatupilia mbali maombi ya baba wa marehemu, hivyo inaamuru mwili huo apewe mke wake. 


“Maombi ya baba wa marehemu yanatupiliwa mbali, Mahakama inaamua mwili huo uzikwe walikozikwa watoto wake waliofariki dunia,”alisema. 


Hakimu Sachore alisema katika kesi hiyo, Wakili wa utetezi, Daniel Buma alidai marehemu anatakiwa azikwe mkoani Tanga kwa madai kuwa ndiyo mila zao zinavyoeleza kwa sababu hana makazi ya kudumu Dar es Salaam. 


Hata hivyo, Mahakama ilipokea vielelezo kutoka kwa mlalamikiwa (Glory) ambavyo ni cheti cha ndoa na picha za watoto wao waliokufa na vyeti vya watoto waliopo. 


Baada ya kutolewa uamuzi huo, Glory alibubujikwa machozi ya furaha na kuomba Mahakama impe ulinzi wakati wa mazishi ya mumewe yanayotarajia kufanyika leo katika makaburi ya Yombo Vituka.



Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top