CHADEMA wamjibu Msajili wa Vyama vya Siasa juu ya tuhuma za kutumia matusi, uongo, uchochezi

Baada ya kulifanyia uchambuzi na kulitafakari tamko la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lililotolewa jana na msajIli mwenyewe, Jaji Francis Mutungi tumeona ni jambo lenye afya kwa ustawi wa demokrasia nchini, kusahihisha upotoshaji uliomo katika taarifa hiyo ili kuendelea kumsaidia msajili na watu wengine, watawala na walio sehemu ya utawala, kuelewa matakwa na maslahi ya wananchi hasa katika wakati huu ambao taifa linapitia.

Kwa hakika tumeshangazwa na kauli zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, kutokana na jinsi ambavyo anaanza kuonesha kuyumba katika kutimiza wajibu wake hasa kwa kutumia weledi na ujuzi wake wa sheria kwa kiwango cha nafasi yake kama jaji.

Katika tamko lake alilolitoa jana na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari jana hiyo na leo, ameshindwa kuonesha neno hata moja linaloashiria matusi, kashfa, uongo au hata kuvuruga amani lililotolewa mbele ya waandishi wa habari juzi wakati Chama kikisoma hadharani maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu.

Ni jambo la kushangaza kuwa Msajili Mutungi, Jaji wa Mahakama Kuu ameweza kuweka vifungu vingi vya kisheria akidai kuwa vimevunjwa lakini hawezi kuonesha ushahidi wa namna vilivyovunjwa au maneno yanayothibitisha kuvunja hizo sheria. 

Hii si sahihi hata kidogo na inakuwa ‘serious’ zaidi inapofanywa na mtu mwenye weledi wa sheria wa kiwango cha Jaji Mutungi.

Wakati Jaji Mutungi akinukuu vifungu vya sheria na kanuni akionekana dhahiri kuwa kuegemea na kuwatetea watawala ambao wamedhihirisha kuwa wanatamani nchi irudi enzi za ‘ujima’ wa fikra za chama kimoja, kwa sababu anazozijua mwenyewe amesahau au ameshindwa au amefanya makusudi kwa sababu anazozjijua mwenyewe, kunukuu kifungu cha 4(1) (e) cha maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007, ambacho kinatoa haki kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano kwa mujibu wa sheria.

Tulidhani kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye si tu kwamba ni mlezi wa vyama vyote bali pia anasimama kama mwamuzi wa mchezo wa mpira uwanjani, katikati ya timu mbili uwanjani, angelisimamia kifungu hicho muhimu na kukitumia kuwakemea na kuwaonya watawala, akiwemo Rais, Waziri Mkuu na Jeshi la Polisi wasivunje sheria za nchi kuzuia shughuli za siasa nchini kwa sababu yoyote ile kwa sababu hawako juu ya sheria za nchi hii.

Aidha, sasa tunaanza kushtuka na kuanza kujiuliza maswali mengi kuhusu kasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kujijengea utaratibu usiokuwa na kawaida kwa nafasi yake ya kisiasa na kisheria, kuwa na kasi ya ajabu kutoa kauli au matamko yanayoonesha kuwatetea/kuwalinda watawala wanapovunja sheria zinazosimamia vyama vya siasa. 

Jaji Mutungi amekuwa mahiri wa kuvikemea au hata kuvionya vyama vingine tofauti na CCM, kila vinapodai haki za kisiasa ambazo ziko na zinapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, wala si kwa hisani ya mtu yeyote.

Waandishi wa habari na umma kwa ujumla watakuwa mashahidi kwa namna ambavyo CCM wamekuwa wakitumia vyombo vya dola, kuvikandamiza, kuvinyanyasa, kuviwekea mazingira magumu na kuvinyima haki za kufanya siasa vyama vingine washindani wake kwa ajili tu ya kulinda maslahi ya chama kilichoko madarakani.

Katika hali hiyo ambayo hata imekuwa ikisababisha mauaji na umwagaji damu za watu wasiokuwa na hatia kwa sababu tu ni wafuasi wa vyama vingine, Msajili wa Vyama vya Siasa hajawahi kuthubutu kujitokeza hadharani kuwaonya na kuwakemea CCM na walioko serikalini kuwa kutumia vyombo vya dola kwa manufaa yao ya kisiasa ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi kupitia kifungu cha maadili ya vyama vya siasa cha 5(1)(c), za mwaka 2007.

Tulitegemea kwa kutumia umahiri huo huo wa kunukuu vifungu vya sheria na kanuni za maadili ya vyama vya siasa ambao Msajili amekuwa akiuonesha dhidi ya vyama washindani wa CCM kila vinapodai haki za msingi za kisiasa, angekuwa ameutumia pia kuwakemea, kuwaonya au hata basi kuwakumbusha CCM na Rais Magufuli kwa kutumia kifungu cha 5(1) (i) cha kanuni za maadili ya vyama vya siasa za Mwaka 2007, kuwa ni makosa kutumia mamlaka, rasilimali za serikali, vyombo vya dola au wadhifa wa kiserikali, kuvikandamiza vyama vingine kwa manufaa ya kisiasa ya upande mmoja.

Si hayo tu, Jaji Mutungi ama aliamua kuwa kimya au alikuwa na kigugumizi aliposikia;
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais John Magufuli na Jeshi la Polisi wakitoa kauli kinyume cha sheria wakitangaza na kuagiza kuzuia shughuli za kisiasa nchini kwa matakwa yao tu.
Mabalozi na wanadiplomasia wakizuiwa kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa.
Kukiukwa kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu za nchi katika uteuzi wa wakurugenzi na makatibu tawala.
Hali tete inayoendelea Zanzibar baada ya watawala kuharibu uchaguzi mkuu mwaka jana kisha wakafanya uchaguzi wa marudio kwa maslahi ya CCM, kinyume kabisa na sheria za nchi.
Hayo ni baadhi tu ya masuala ya muhimu ambayo ofisi ya msajili ilitarajiwa kuwa ingekuwa mstari wa mbele kukemea na kuonya ili kuweka mizania ya ushindani wa kisiasa katika usahihi wake.

Kwa mwenendo huu ambao usipoangaliwa na kufanyiwa kazi ya kuurekebisha haraka, tunachelea kusema kuwa Ofisi ya Msajili na Jaji Mutungi mwenyewe wataanza kujikosesha uhalali machoni pa Watanzania ambao wasingependa kuona siasa ambayo ni maisha yao, ikifananishwa kama vile ni jambo la kawaida tu lisilokuwa na maana.

Kupitia taarifa hii, tunamtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi kuwa makini na utaratibu huo vinginevyo Watanzania wataanza kuiweka ofisi yake na yeye mwenyewe kwenye kapu moja na aliyekuwa mtangulizi wake, ambaye ilifika mahali wananchi walimuona yeye binafsi, kupitia kauli zake, matendo yake na ofisi yake kwa ujumla, sawa na sehemu ya chama kilichoko madarakani.

CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani nchini hakiwezi kuvumilia wala kukubali hiki kinachoanza kujionesha kuwa ni ‘double standards’za mtu anayetarajiwa kuwa mlezi na refarii, kujitokeza hadharani pale tu ambapo maslahi ya chama tawala na watawala yanapoguswa lakini anakuwa kimya na hata kuweka masikio nta mara vyama washindani wa CCM vinapokandamizwa, kinyume kabisa cha sheria.

Kama chama chenye wanachama na viongozi wanaojua haki na wajibu wao wa kikatiba na kisheria, tutaendelea kufanya shughuli za kisiasa kwa namna itakayosimamia haki na matumaini ya wananchi kwa ajili ya amani na utulivu wa kweli, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi si kwa kufuata matamko, kauli au maelekezo ya mtu yeyote.

Ni kwa kuzingatia dhana hiyo, maana Kamati Kuu katika kikao cha dharura kilichofanyika mwishoni mwa juma lililopita na maazimio yake kutangazwa juzi Jumatano, moja ya maazimio yake ni kuanzisha operesheni ya UKUTA (Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania) ambayo inalenga kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali tofauti zao zozote zile, kudai haki na matumaini dhidi ya udkiteta katika nchi yao na kuzuia harakati za watawala kuataka kupora mamlaka ya wananchi na kujiweka juu ya sheria kwa namna ile ile ambayo madikteta hufanya.

Imetolewa leo Ijumaa Julai 29, 2016 na;
Prof. Mwesiga Baregu
Mjumbe wa Kamati Kamati Kuu

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top