Aliyeoongoza kidato cha 6 ni tunda la Shule ya Kata, aeleza alivyodharauliwa



Mwanafunzi aliyeongoza katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Hassan Gwaay ameonesha moja kati ya tunda bora lililodhihirisha faida ya kuanzishwa
kwa shule za kata na Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Dk. Jakaya Kikwete.


Gwaay mwenye umri wa miaka 19 ameeleza kuwa alisoma katika shule ya kata ya Mirerani Benjamin W. Mkapa mkoani Manyara alipopata elimu ya kidato cha nne na kupata ufaulu mzuri uliomuwezesha kuchaguliwa kujiunga na shule ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys) kuendelea na elimu yake ya kidato cha tano.


Amesema kuwa alipokuwa akisoma katika shule hiyo ya kata, wanafunzi waliokuwa wanasoma katika shule za watu binafsi zenye mazingira bora zaidi ya walikuwa wakimuonesha dharau lakini alitaka kuwadhihirishia kuwa hata katika shule hiyo anaweza kufanya vizuri zaidi yao.


“Sikujali kelele na dharau za watoto waliosoma kwenye shule za kulipia, ambao mara kwa mara walikuwa wakiibeza shule yetu. Nilopomaliza kidato cha nne, nilipata daraja la kwanza alama 10 (Division 1 ya point 10). Ndipo nilipowadhihirishia kuwa hata kwenye shule za kata watu wanafaulu,” Gwaay anakaririwa na gazeti la Jambo Leo.


Mwanafunzi huyo ambaye amelelewa na bibi yake kwa muda mrefu baada ya mama yake kufariki huku akiishi mbali na baba yake (anamsapoti), alisema kuwa baada ya kujiunga na shule ya wavulana ya Tabora kusoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM), aliweka bidii zaidi hasa baada ya kugundua kuwa wanafunzi aliokutana nao hapo wote walikuwa na akili sana.


Alisema kuwa alipofanya mtihani wa ‘Mock’ alipata Fizikia (A), Kemia (A) na Hesabu (B) na kwaba aliumia sana kuona amepata B. Aliongeza bidi hadi kuibuka na alama A kwenye mitihani yote katika Mtihani wa Taifa na kutangazwa kuwa mwanafunzi aliyeongoza.


Changamoto ya upungufu wa walimu hususan wa Sayansi katika shule nyingi za umma nchini lilimkumba pia Gwaay katika shule ya wavulana ya Tabora, lakini aliipanda ngazi hiyo ndefu kwa nguvu ya ziada bila kukata tamaa.


“Hakuwa na Mwalimu wa Fizikia pale. Tangu najiunga sikuwahi kumwona zaidi ya wakuazimwa ambaye alikuwa akija jioni na mwisho mwa wiki tu na alikuwa akija mara chache. Muda mwingi tulitumia kujisome wenyewe lakini hatukukata tamaa,” alisema.


Shule ya wavulana ya Tabora mwaka huu imerudi kwenye nafasi yake ya ubora ulioaminika miaka mingi iliyopita. Imeshika nafasi ya 5 kati ya shule zote. 

Post a Comment

Toa maoni tu (kejeli na matusi marufuku)

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top