Serikali Kuweka Pingamizi Dhidi ya Maombi ya Kulishitaki Jeshi la Polisi Yaliyofunguliwa na CHADEMA


Serikali inakusudia kuweka pingamizi dhidi ya maombi ya kulishtaki Jeshi la Polisi katika kesi yaliyofunguliwa na Chadema jijini Mwanza.

Hayo yalielezwa jana na jopo la mawakili watatu wa Serikali, Robert Kidando, Obadia Kajungu na Seti Mkemwa wakati shauri hilo lilipotajwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa.


Kutokana na kusudio hilo, Jaji Matupa anayesikiliza shauri hilo namba 87 la mwaka 2016, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 28 kutoa fursa kwa upande wa utetezi kuwasilisha hoja zake.

Katika shauri hilo ambalo ni la tatu kufunguliwa na chama hicho, Chadema inawakilishwa na mawakili Gasper Mwanaliela, John Mallya na Paul Kipeja.


Kwa mara ya kwanza, Chadema kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ilifungua kesi Juni 10, dhidi ya wadaiwa wanne, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi Nsato Mssanzya, wakuu wa polisi wilaya za Geita na Kahama na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Chama hicho kiliwaondoa Kamishina Mssanzya na OCD wa Kahama kutokana na hitaji la kisheria kuelekeza washtakiwe katika maeneo yao au Masjala Kuu ya Mahakama jijini Dar es Salaam.


Juni 15, Chadema ilifungua upya shauri hilo kwa kuwabakisha wadaiwa wawili OCD wa Geita na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Hata hivyo, shauri hilo lilifutwa kukubaliana na pingamizi la upande wa utetezi kwamba lilifunguliwa kupitia Kanuni ya 5(3) badala ya 5(1)(2) ambayo ingeipa mahakama mamlaka ya kuisikiliza na kuiamua.


Katika uamuzi wake, Jaji Gwae alitoa fursa kwa Chadema ama kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake au kurekebisha kasoro hiyo kupitia kanuni ya 17 na kuirejesha mahakamani.

Mawakili wa Chadema walirekebisha kasoro hiyo na kurejesha upya shauri hilo.


Chadema inaiomba Mahakama kutamka kuwa zuio la polisi na utekelezaji wake ni batili kwa sababu inakiuka Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inayoruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa ikiwamo maandamano na mikutano ya hadhara.


Chama hicho pia kinaiomba Mahakama itoe katazo kwa jeshi la polisi kwamba lisitoe amri kama hiyo na kuruhusu vyama vya siasa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara huku polisi wakiamuriwa kulinda usalama kama sheria inavyoelekeza. 
Newer Posts Older Posts
© Copyright UCHAMBUZI LEO | Modified By Smart WEB
Back To Top Back To Top